Habari za Kitaifa

Mudavadi asisitiza Chebukati anatosha kuwa Jaji Mkuu

February 6th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

MKUU wa Mawaziri Musalia Mudavadi sasa anamtetea mwenyekiti wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Wafula Chebukati kwamba ana haki ya kuwasilisha jina lake kwa uteuzi kuwa Jaji Mkuu nchini.

Akiongea mjini Kakamega mnamo Jumapili wakati wa ibada ya pamoja iliyohudhuriwa na Rais William Ruto, Bw Mudavadi alimshambuliwa kinara wa Azimio Raila Odinga kwa kumsuta Rais Ruto kwamba anapanga njama ya kuhakikisha Chebukati anateuliwa Jaji Mkuu kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027.

Kwenye kikao na wanahabari ofisini mwake katika jengo la Capitol Hill, Bw Odinga alisema kuwa kuna njama ya kumteua Bw Chebukati kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufaa kisha apandishwe ngazi hadi Jaji Mkuu kabla ya 2027.

“Tumepata habari kwamba mojawapo ya ajenda za mkutano kati ya Jaji Mkuu Martha Koome na Ruto katika Ikulu ya Nairobi ilikuwa na kuhakikisha uteuzi wa majaji watakaopendelea serikali. Miongoni mwa wanaoratibiwa kuteuliwa ni wenyeviti wa zamani wa IEBC Isaack Hassan na Wafula Chebukati,” akasema Bw Odinga akiwa ameandamana na maseneta Edwin Sifuna (Nairobi) na Godffrey Osotsi (Vihiga).

Baada ya mkutano huo wa Ikulu ambao pia ulihudhuriwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula na mwenyekiti wa Baraza la Magavana Anne Waiguru, Jaji Mkuu Koome alitangaza kuwa majaji 11 wataajiriwa katika Mahakama ya Rufaa na watano wataajiriwa katika Mahakama Kuu.

Lakini Jumapili Mudavadi akasema: “Tume ya Huduma za Bunge ni asasi huru na inayo haki ya kuajiri mtu yeyote aliyehitimu kuwa Jaji. Ni makosa kwa Azimio kuanza kupendekeza wale ambao wanastahili kuajiriwa na wale hawafai. Hata kama Bw Chebukati atateuliwa kuwa Jaji Mkuu, hiyo ni haki yake na amehitimu,” Bw Mudavadi akasema.

“Huwezi kutuambia kuwa mtu akitaka kuwa Jaji, hata kama ni Bw Chebukati au mwingine, hafai kuteuliwa. Ni wajibu wa JSC kuteua mtu aliyehitimu kuwa Jaji au hata Jaji Mkuu. Kuna makosa gani Bw Chebukati akiteuliwa kuwa Jaji Mkuu?” Mudavadi, ambaye pia ni Waziri wa Masuala ya Kigeni akauliza.

Jaji Mkuu Koome ambaye aliteuliwa mnamo 2022 akiwa na umri wa miaka 65 anaruhusiwa na Katiba kuhudumu kwa miaka mitano hadi atakapotinga umri wa miaka 70.

Lakini tayari Mkenya mmoja amewasilisha ombi kwa JSC akitaka Bi Koome afutwe kazi.

Majaji wanahitajika kustaafu baada ya kutimu umri wa miaka 70.

Bw Odinga alidai mkutano wa Ikulu ulilenga kuhakikisha kuwa serikali kuu inayoongozwa na Rais Ruto inadhibiti Idara ya Mahakama.