• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Murkomen adai mapaa yanavujisha maji JKIA kwa sababu serikali ya Uhuru ilifanya kazi duni

Murkomen adai mapaa yanavujisha maji JKIA kwa sababu serikali ya Uhuru ilifanya kazi duni

NA SIAGO CECE

WAZIRI wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen amesema mapaa yanayovujisha maji katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), ni matokeo ya kazi duni ya mkandarasi na wahandisi waliokuwa wakifanya ukarabati katika sehemu za Terminal 1C na 1E.

Ameilaumu serikali iliyotangulia ya Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta akisema ‘ililala darasani’.

Bw Murkomen alisema ukarabati uliofanywa baada ya sehemu ya JKIA kushika moto miaka michache iliyopita, ulikuwa duni na ulifanywa bila kukidhi viwango vinavyohitajika.

Waziri wa Uchukuzi Kipchumba Murkomen akikagua uwanja wa ndege wa Diani, Kaunti ya Kwale mnamo Novemba 14, 2023. PICHA | SIAGO CECE

Akizungumza Jumanne katika uwanja wa ndege wa Diani katika Kaunti ya Kwale alipokuwa akikagua upanuzi wa uwanja huo, Bw Murkomen alisema ukarabati huo utafanywa upya kukidhi viwango vinavyohitajika.

“Tulipoingia ofisini, tuligundua kuwa miradi ya serikali iliyopita ilikuwa dhaifu. Ukarabati huo ulipofanywa kwenye Kituo cha 1C na E, ulikuwa wa haraka. Lakini tumezungumza na wakandarasi ili wafanye kazi upya,” Bw Murkomen alisema.

Alisisitiza kwamba wahandisi na mkandarasi waliokuwa wakisimamia ukarabati huo watalazimika kuelezea kwa nini kulikuwa na kazi mbovu iliyosababisha maji ya mvua kuvuja mnamo Jumatatu.

“Watalazimika kueleza kwa nini mvua kubwa inaponyesha lazima paa livujishe maji,” Bw Murkomen akasema.

Hata hivyo alisema mapaa yanayovuja yamerekebishwa kwa muda ili kuzuia kuvuja zaidi katika msimu huu wa mvua.

Waziri huyo alisema mkandarasi mpya atapewa kazi ili kujenga sehemu mpya ya uwanja wa ndege.

Mkataba huo utakuwa wa kati ya mwekezaji wa kibinafsi na serikali na ambao utaanza Januari 2024.

“Tayari tumeanza kujitayarisha na Rais William Ruto amesema inabidi tumalize kujenga uwanja mpya wa ndege ifikapo 2027,” Bw Murkomen akaahidi.

Kuhusu usambazaji wa kawi katika Uwanja wa Ndege Bw Murkomen alisema kuwa serikali tayari imesuluhisha changamoto ya stima kupotea kwa kuweka jenereta lakini bado ukarabati haujamalizika kuhakikisha kuwa stima haipotei kwa zaidi ya sekunde 30.

Alisema njia ya kupishana umeme kwa sasa inachukua dakika 20 lakini wanajitahidi kuhakikisha wanapunguza muda hadi sekunde 30.

Mwango Capital ambao walichapisha video ikionyesha mapaa yakivujisha maji, walisema Jumanne wanashangaa namna serikali ya Kenya Kwanza imezembea kwa mwaka mzima tangu iingie madarakani mnamo Septemba 13, 2022.

“Waziri wa Uchukuzi @kipmurkomen ametoa kauli yake baada ya kuona video ambayo tulirekodi na kuchapisha Jumatatu ikionyesha mapaa yakivujisha maji JKIA akiilaumu serikali iliyotangulia. Hata hivyo, hii serikali imekuwa uongozini kwa mwaka mmoja, na utepetevu umekuwepo kipindi hicho chote,” wakachapisha kwa mtandao wa X.

Tazama video yenyewe hapa chini.

  • Tags

You can share this post!

UoN na mwanakandarasi wazozania malipo ya ujenzi wa mabweni...

Kivutio maarufu kwa watalii Kisumu ambacho kimegeuka Sodoma...

T L