Michezo

Murkomen ashtakiwa kuhusu usimamizi wa riadha

Na RICHARD MUNGUTI August 31st, 2024 2 min read

JITIHADA za walalamishi wanne kumshurutisha Waziri wa Michezo, Kipchumba Murkomen kuunda kamati ya muda kusimamia riadha  hazijafaulu.

Hata hivyo Jaji John Chigiti, aliwaagiza walalamishi Casper Cheruiyot, Evans Ayienda Siro, John Mwania Nzau na Edward Mburu Mwaura Agosti 28,2024 wamkabidhi Murkomen na nakala za kesi waliyomshtaki ajibu madai kwamba sekta ya riadha inakumbwa na matatizo ya usimamizi.

Walalamishi hawa waliamriwa wamkabidhi Murkomen na nakala za kesi yao ndipo awasilishe majibu katika muda wa siku 14 kuanzia Agosti 28,2024 kufuatia kwamba riadha inakumbwa na matatizo makubwa na maamuzi yanayochukuliwa sasa yanakaidi haki za wanariadha na wengine wanaohitimu kushiriki katika fani hii ya michezo.

Katika kesi waliyowasilisha Mahakama kuu Cheruiyot, Siro, Nzau na Mwaura wamelalamika kwamba maamuzi yanayochukuliwa na wasimamizi wa kamati ya riadha hayafaidi wanaspoti na yanakaidi haki zao.

Walalamishi hawa wanne wamesema Katiba na Sheria nambari 54 za Michezo inamjukumisha Waziri wa Michezo kuteua kamati ya kusimamia kitengo chochote cha michezo kinachokumbwa na mtafaruku wa usimamizi.

Imefafanuliwa katika ushahidi uliowasilishwa mbele ya Jaji Chigiti kwamba endapo mahakama kuu haitaingilia kati na kutoa mwelekeo fani hii ya spoti inayoletea nchi sifa sufufu itaendelea kudhoofika na hatimaye kusambaratika.

Mahakama pia imeombwa iamuru Katiba ya Athletics Kenya ifanyiwe mabadiliko iambatane na hali ya sasa ya riadha.

Cheruiyot, Siro, Wanzau na Mwaura wameomba mahakama kuu imwamuru Msajili wa Spoti aitishe mkutano wa uchaguzi wa Athletics Kenya katika muda wa siku 90.

“Katiba ya 2010 inaagiza kuwe na usimamizi wa sekta ya spoti na Kifungu nambari 54 cha Sheria za Spoti kinamruhusu Waziri wa Michezo kuteua kamati ya kusimamia fani ya michezo inayosimamiwa vibaya,” wanne hao wanasisitiza.

Wanne hao Cheruiyot, Siro, Wanzau na Mwaura wamewashtaki Waziri wa Michezo (Murkomen), Katibu Mkuu Wizara ya Michezo, Wizara ya Michezo, Kamati Kuu Athletics Kenya na Msajili wa Michezo.

Wanne hao wameomba mahakama kuu iamuru Murkomen asimamie barabara fani ya Michezo.

Jaji Chigiti aliwaagiza wahusika wote wawasilishe ushahidi wote na wafike mbele yake Novemba 28,2024 kuelezwa siku ya uamuzi mkuu.

[email protected].