Habari Mseto

Mvurya apinga matamshi ya Linturi, ataka muguka izimwe Pwani

June 13th, 2024 1 min read

Na KNA

WAZIRI wa Madini na Uchumi wa Baharini, Bw Salim Mvurya, ameunga mkono shinikizo linaloendelezwa na viongozi wa Pwani dhidi ya uraibu wa muguka.

Akizungumza katika upanzi wa miche 60,000 ya mikoko Kipini, Kaunti Ndogo ya Tana Delta, Bw Mvurya alisisitiza haja ya kuwepo kwa sheria kali ya kuwalinda vijana dhidi ya muguka ambayo utafiti umethibitisha ni dawa ya kulevya.

Amesema haya siku moja baada ya Waziri wa Kilimo Mithika Linturi, kuvunja kimya kuhusu mzozo wa muguka unaoendelea nchini, katika hafla Embu, alipopinga kupigwa marufuku kwa muguka, akikiri kuwa ni zao halali ambalo halipaswi kukataliwa.

“Nguvu ile inayotumika dhidi ya pombe haramu na dawa za kulevya inapaswa kutumika pia kwa muguka,” alisema.

Kuhusiana na mjadala wa kugawana mapato kwa kuzingatia zaidi idadi ya watu katika eneo, Waziri alielezea wasiwasi wake kwamba utazitia hasara kaunti zilizotengwa kihistoria kama vile Tana River.

Bw Mvurya alizitaka jamii kushiriki kikamilifu katika mpango wa upandaji miti.

“Zoezi la upandaji miti ni hatua kubwa ya kufikia malengo kukabiliana na athari mbaya za mabadiliko ya tabianchi. Upandaji wa miti ya mikoko Kipini ni wazo zuri linalolenga hayo,” alisema Bw Mvurya.

Aidha, Mvurya alitangaza kuwa mipango inaendelea ya kujenga eneo la kutua samaki humo, ili kuimarisha sekta ya uvuvi.