Habari Mseto

MAWAIDHA YA KIISLAMU: Daima fikiria na upime maneno kabla ya kuyatamka

January 26th, 2024 2 min read

NA HAWA ALI

SIFA zote njema anastahiki Mwenyezi Mungu Subuhaanahu wata’ala, mwingi wa rehema na mwenye kurehemu.

Swala na salamu zimwendee mtume wetu Muhammad swalla Allahu a’alayhi wasallam, swahaba zake kiram na watangu wote wema wote hadi siku ya kiyamaah.

Miongoni mwa baraka za Mwenyezi Mungu Subuhaanahu wata’ala juu ya mwanadamu ni kwamba amemfanya mtu mwenye akili timamu na akamuumbia ulimi.

Alimfanya aweze kutoa sauti na kufafanua anachotaka kupitia maneno anayozungumza. Inabidi azungumze tu ili watu wajue anachotaka.

Hivyo, tunapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu Subuhaanahu wata’ala kwa baraka alizotuneemesha. Tunapaswa kutumia semi zetu kwa njia zenye manufaa; si kusema bali wema.

Kwa mfano, ikiwa tuko kwenye mkutano au mkusanyiko na tunataka kuzungumza na watu, au mjadala wowote unakuja basi tunapaswa kufikiria kwanza kile tunachotaka kusema na kuchagua maneno gani ya kutumia.

Ikiwa tunaweza kutoa mashauri yenye manufaa kwa watu, tunapaswa kusema kwa njia hiyo ili kuwafanya watu wengine watake kusikiliza.

Kwa hivyo, maneno yako yatakubaliwa kwa Mwenyezi Mungu Subuhaanahu wata’ala na watu kwa sababu maneno yako yana manufaa katika kuongoa kwenye wema au kupatanisha watu, au kufundisha elimu yenye manufaa, na yatazidisha mapenzi ya watu wao kwa wao.

Tukisema neno la kheri tutapata malipo ya Mwenyezi Mungu na mapenzi na heshima ya watu na hivyo tutashinda.

Mtume swalla Allahu a’alayhi wasallam alisema: Ikiwa mwanadamu hawezi kusema jambo la manufaa, basi anyamaze na kunyamaza kwake kutamweka mbali na ghadhabu ya Mwenyezi Mungu Subuhaanahu wata’ala na madhara yanayoweza kumpata kutokana na kusema maneno mabaya.

Mwenye kuwafanyia watu maovu, basi watu watamkabili kwa uovu pia. Na hakika ukisema maneno mabaya yanaweza kukuletea matatizo na madhara na kukufanya ujute na kutamani ungekaa kimya.

Hivyo basi, Mtume swalla Allahu a’alayhi wasallam anatuelimisha kwa tabia njema akisema: Ama zungumza neno lenye manufaa na zuri, au unyamaze ambalo ni bora kwako kuliko kusema maneno maovu.