Makala

Mwalimu adaiwa kujinyonga kwa kupoteza Sh50,000 kwa Aviator

June 6th, 2024 2 min read

NA WYCLIFFE NYABERI

MWALIMU wa Shule ya Upili ya Wavulana ya Nyamira ameaga dunia baada ya kudaiwa kujitia kitanzi alipopoteza pesa kwenye mchezo wa kamari unaofahamika kama ‘Aviator.

Aviator ni mchezo wa kamari unaochezwa mitandaoni na una dhana rahisi ya kuvutia ambapo wachezaji huweka dau na kutazama kadri kizidishi kinavyoongezeka muda unavyopita.

Kizidishi hicho kinafanana na ndege. Kadri ndege hiyo inavyozidi kupaa ndivyo pesa za mchezaji zinaongezeka.

Ili kushinda katika mchezo huo, mteja anafaa kuziondoa pesa zake kabla ya kizidishi kuporomoka. Ikiwa mchezaji ataacha kizidishi hicho kiporomoke, basi hela zake zitakuwa zimezama na hivyo basi kuendelea, mchezaji hulazimika kutumia kiasi kingine cha pesa.

Wakati mwingine, mchezaji hupata wakati mgumu kuondoa pesa zake zikiwa nyingi hata akibonyeza kitufe cha kuziondoa.

Kulingana na Naibu Chifu wa Nyamira Mjini Bw Johnson Manyara, marehemu aliyetambuliwa kama Kelvin Omwenga,30, anasemekana kujinyonga katika nyumba yake ya kupanga mnamo Jumatano usiku.

“Inasemekana alichukua uamuzi wa kujitoa uhai baada ya kupoteza Sh50,000 kwenye kasino hiyo ya Aviator,” Bw Manyara akasema.

“Nilifahamishwa hayo na wananchi. Mara moja nilielekea nyumbani kwake na kukuta mwili wake ukining’inia darini. Niliwafahamisha polisi mara moja na wakakuja kuutoa mwili na kuupeleka katika chumba cha kuhifadhia maiti huku uchunguzi kuhusu tukio hilo ukiendelea,” akaelezea.

Naibu chifu huyo aliongeza kuwa mke wa mwalimu huyo hakuwa nyumbani.

“Alijifungua hivi karibuni na hakuwepo nyumbani wakati tukio hilo la kusikitisha lilitokea. Alikuwa amesafiri kwenda mashambani baada ya kujifungua. Pia walikuwa wamearifiwa kwamba wazazi wao walikuwa wagonjwa na kwa hivyo, mwalimu alikuwa amemwambia mke aende kuona jinsi wanavyoendelea,” Bw Manyara akaongezea.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Nyamira Bw George Onkundi alisema walishangaa kusikia kifo cha Bw Omwenga kwa njia hiyo.

Mkuu huyo alibaini kuwa marehemu alikuwa ameajiriwa na Bodi ya Wasimamizi wa shule hiyo (BOM) na alikuwa amekaa nao kwa miaka minne.

“Alikuwa akifundisha masomo ya Hisabati na Kemia. Alikuwa amekaa nasi kwa miaka minne. Hakuripoti kazini Jumatano. Kifo chake kimetushtua,” Bw Onkundi alisema.

Mkuu huyo aliongeza kuwa marehemu hakuwahi kuonyesha dalili zozote za msongo wa mawazo. Lakini alithibitisha kuwa marehemu alikuwa akikopa pesa kutoka kwa wenzake.

“Hakuonyesha dalili zozote za msongo wa mawazo lakini alikuwa ametaja kuwa kuna masuala ambayo yalikuwa yakimsumbua nyumbani. Mara nyingi alikuwa akipokea usaidizi wa kifedha kutoka kwa walimu wenzake lakini haikuwa imefikia wakati wa kumtaka kulipa madeni,” akasema.

Mwalimu mwingine katika shule hiyo, Bw Pethuel Mong’are, alisema marehemu alikuwa akimkopa pesa mara kwa mara huku akiahidi kuwa atazirudisha kwa wakati ufaao.

“Alikuja kwangu na kuniomba mkopo. Alinipa mpango wa jinsi ambavyo angenilipa kidogokidogo hadi wakati ambapo angemaliza deni kikamilifu. Mara ya mwisho nilipozungumza naye ilikuwa Jumanne. Pia nimeshtuka kusikia kuhusu kifo chake. Siwezi kusema kikamilifu kwamba aliaga dunia kwa njia hiyo lakini hili ni suala ambalo polisi wanafaa kuchunguza na kutueleza kilichotokea,” Bw Mong’are aliongeza.