Habari za Kitaifa

Mwalimu Dida, aliyewahi kuwania urais, atumikia jela miaka 7 Amerika


MOHAMED Abduba Dida, mwalimu wa zamani ambaye aligombea urais mara mbili na kumaliza mbele ya baadhi ya wanasiasa mashuhuri, anatumikia kifungo cha miaka saba katika jela moja Amerika kwa kunyemelea mtu  na kutoa vitisho.

Dida anazuiliwa katika gereza la Big Muddy, Illinois, ambako amekuwa tangu Novemba 18, 2022 baada ya kupatikana na hatia ya kumnyemelea na kumtisha mtu asiyejulikana katika jimbo la Magharibi mwa Amerika.

Japo  wakati wa kuchapisha habari hii Taifa Leo haikuwa imethibitisha kuhusu mlalamishi, rekodi katika gereza la Muddy zinaonyesha kuwa mgombea huyo wa zamani wa urais alipatikana na hatia kwa mashtaka mawili tofauti.

Alitekeleza makosa hayo  katika Kaunti ya Mclean, Illinois.

Katika shtaka la kwanza, Dida alipatikana na hatia ya kunyemelea na kutoa vitisho dhidi ya mlalamishi. Kwa kosa hili, alihukumiwa miaka miwili jela.

Katika shtaka la pili, Dida alipatikana na hatia kwa kosa moja la kunyemelea na kukiuka agizo  ambalo lilimzuia kumkaribia au kuzungumza na mlalamishi.

Mohamed Abduba Dida, aliyekuwa mwalimu ambaye aliwahi kuwania urais 2013 na 2017. Dida anatumikia kifungo cha miaka saba katika jela moja Amerika. Picha| Big Muddy Correctional Center, Illinois

Kwa shtaka hili, Dida alihukumiwa kifungo cha miaka saba jela.

Alifungwa gerezani Julai, 2021 lakini hukumu hiyo iliongezwa katika hali isiyoeleweka.

Dida anatarajiwa kutoka gerezani Aprili 3, 2029.

Ombi ambalo amewasilisha kutaka uhuru wa kutekeleza kanuni za dini yake,  linaonyesha kuwa Big Muddy ni gereza la tatu kumzuilia Dida.

Kufungwa jela kwake kunaonyesha tofauti  kubwa kwa mtu ambaye aliendesha kampeni ya  maadili na taifa lisilo na ufisadi katika harakati zake za kuwania urais.

Mwezi mmoja kabla ya Uchaguzi Mkuu wa Machi, 2013, Dida alitangazwa kuwa mgombeaji mpya zaidi katika kinyang’anyiro cha kuwania urais, akipeperusha bendera ya Alliance for Real Change, mgombea mwenza wake alikuwa Joshua Odongo.

Mjadala wa urais uliotangazwa na vyombo vingi vya habari,  ulimfanya Dida kuwa mtu mashuhuri kwa usiku mmoja kwani majibu yake kwa masuala ya utawala kama vile rushwa yaliwavutia watazamaji wengi.

Katika mahojiano na runinga ya Citizen, Dida alisema kuwa kama Daudi, angemrushia jiwe moja na kumwangusha Goliath, ambaye katika muktadha huu walikuwa wagombea wengine wote wa urais, akiwemo Uhuru Kenyatta na Raila Odinga.

Katika uchaguzi huo,  Dida alimaliza wa tano kwa kura 54,840. Lakini matokeo yake yalikuwa bora kuliko ya wanasiasa wawili mashuhuri kama aliyekuwa waziri wa Sheria Martha Karua (kura 43,881) na aliyekuwa Mbunge wa Kabete Paul Muite (kura 12,580).

Katika kampeni hiyo, Dida aligonga vichwa vya habari tena alipokataa maafisa wawili wa polisi waliotumwa kumhudumia, badala yake alitaka walinda usalama 20. Ombi hilo lilikataliwa.

Katika uchaguzi wa 2017, Dida alimaliza wa nne kwa kura 38,004 na bora zaidi ya mbunge wa zamani wa Lugari Cyrus Jirongo.

Mnamo Aprili 15, 2024 Dida aliwasilisha ombi dhidi ya Kimberly Hvarre, mlinzi wa gereza la Muddy, kwa madai ya ukiukaji wa haki zake za Uislamu.

Jaji Gilbert C Sison,  alisema katika uamuzi wake kwamba haikufahamika iwapo ombi la Dida liliwasilishwa chini ya Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Amerika au Sheria ya Matumizi ya Kidini na Watu Waliozuiliwa (RLUIPA).

Lakini  alikubali kwamba Dida aliibua masuala ya kisheria kwani dini inatambuliwa katika Marekebisho ya Kwanza na RLUIPA.

Hivi sasa, Dida ni Imam wa kujitolea katika Big Muddy na anaruhusiwa kusali mara moja kila Ijumaa.

“Yeye (Dida) analalamika kwamba hawezi kutimiza vipengele muhimu kuhusu  swala yake, kama vile upande anaopaswa kutazama kuswali, sharti la kuosha nafsi yake kabla ya kuswali, na sharti kwamba baadhi ya sala zinafanyika nyakati za usiku. Anakiri kwamba hivi majuzi alihamishwa kutoka seli aliyozuiliwa peke yake, hatua ambayo inapunguza baadhi ya matatizo yake. Hata hivyo, analalamika kwamba anahitaji kuoga mwili wote kila Ijumaa kabla ya sala, lakini licha ya mikutano mingi kuhusu hili, ameweza kupanga hilo,” inasema sehemu ya stakabadhi za mahakama.

Kutokana na mapungufu hayo, Dida alisema alikataa kushiriki Ramadhani mwaka huu.

Hakimu Sison alimuonya Dida kuwa kesi hiyo inaweza kuchukua muda na kuwa  ni mchakato mgumu.