Habari

Mwanablogu Robert alai akamatwa

June 18th, 2019 1 min read

Na MARY WAMBUI na VINCENT ACHUKA

MWANABLOGU Robert Alai amekamatwa jijini Nairobi, siku moja baada ya maafisa wa polisi kumuonya wakimtaka akome kuchapisha picha za waathiriwa wa matukio ya ugaidi.

Wapelelezi kutoka kwa Idara ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) wamemkamata Jumanne asubuhi na kumsafirisha kwa gari hadi makao makuu ya chombo hicho katika barabara ya Kiambu.

Haijabainika wazi ni kwa nini amekamatwa , lakini Jumatatu, Msemaji wa Polisi, Charles Owino alimuonya baada ya yeye kuchapisha kwenye ukurasa wake wa Twitter picha za maafisa walioangamia wakati wa shambulio Wajir.

Bw Owino alikosoa hatua ya mwanablogu huyo kuchapisha picha za maafisa walioangamia akionya kwamba ni jambo lisilovumilika na kwamba angekabiliwa vilivyo.

“Ni kukosa uzalendo pamoja na kwamba ni unyama. Lazima maafisa wetu wapewe heshima wanazostahiki,” akasema Bw Owino.

Alisema kuchapisha picha za wahanga kunaumiza zaidi familia zao.

“Mwanablogu akichapisha picha za aina hii ni sawa na kuunga mkono matukio ya ugaidi,” alieleza.

Kisa

 

Maafisa waliokuwa wameshika doria waliangamia baada ya vilipuzi kuwalipukia eneo la Konton, Kaunti ndogo ya Wajir Mashariki. Maafisa saba waliangamia papo hapo.

Watatu walipata majeraha, lakini mmoja hazijabainika habari zake ingawa Owino alisema wanaendelea kumtafuta.

Tume ya Uwiano (NCIC) nayo kupitia kwa taarifa ilikashifu hatua ya Bw Alai.

“Alai ana uhuru wa kutoa maoni yake, lakini machapisho ya aina hii yanaweza kufasiriwa kama propaganda ya vita katika Katiba ya Kenya. Hivyo tunamtaka aondowe picha hizo katika majukwaa ya mitandao ya kijamii,” ikasema sehemu ya taarifa hiyo ya NCIC.