Makala

Mwanadada stadi katika kulinda wanyamapori anayelimbikiziwa sifa kedekede

Na LUCY MKANYIKA July 31st, 2024 2 min read

TANGU utotoni, Bi Constance Mwandaa amekuwa akiazimia kulinda mazingira na wanyamapori.

Ingawa alizaliwa na kukulia katika eneo lenye migogoro ya wanyamapori katika kijiji cha Sagala, kaunti ya Taita Taveta, alipata hamu ya kutetea haki zao.

Ziara zake katika mbuga ya wanyamapori ya Tsavo zilimpa furaha kubwa na kumtia moyo kuendelea na juhudi zake za uhifadhi.

“Nilikuwa naona wanyamapori mara kwa mara na nilitamani siku moja kufanya kazi karibu nao ili kuwalinda,” akasema.

Kwa sasa, Bi Mwandaa, mwenye umri wa miaka 32, amekuwa mfano wa kuigwa katika kazi hiyo ambayo imekuwa ikiajiri wanaume wengi kuliko wanawake.

Safari yake katika sekta hiyo ya uhifadhi, ilimpatia Tuzo Maalum ya Majaji katika Tamasha la Filamu za Wanyamapori la Pridelands (PWFF) mwaka huu kwa filamu fupi “Portrait of a Ranger: Connie” kutokana na kujitolea kwake kulinda wanyamapori katika eneo la uhifadhi la Tsavo.

Ndoto yake ilianza kuchukua mkondo mwaka wa 2010 aliposhiriki shughuli ya kuajiriwa na Wildlife Works kwa Mradi wa Kasigau Corridor REDD+.

Akiendeshwa na shauku yake ya utotoni, alishiriki zoezi la uajiri na kuajiriwa kufanya kazi na Wildlife Works mwaka wa 2011.

Tangu wakati huo, amekuwa mstari wa mbele akifanya kazi mchana na usiku katika mazingira magumu ili kulinda wanyamapori na mazingira.

Miaka kumi na nne iliyopita, ni wanaume pekee waliokuwa wakizingatiwa kwa kazi hiyo lakini mbali na Bi Mwandaa, walichaguliwa walinzi wengine watatu wa kike.

Hatua hiyo muhimu imepelekea kuendelea kuleta usawa wa kijinsia katika sekta hiyo ya uhifadhi.

“Sisi wanne tulikuwa katika kambi tofauti, tulikuwa tukipigiana simu kujua hali ilivyokuwa. Ilikuwa ngumu, lakini tulikuwa tumeazimia kufanikiwa,” akasema.

Kwa sasa, kuna walinzi wa kike 10 tu dhidi ya wanaume 100, lakini licha ya changamoto hizo, azimio la Bi Mwandaa lilimfanya apande cheo hadi kuwa sajenti na mkufunzi.

Constance Mwandaa, mlinzi wa wanyamapori akionyesha tuzo aliyoshinda majuzi. Picha| Lucy Mkanyika

Kama sajenti, anaongoza na pia kufunza walinzi, akiwapa maarifa kutokana na uzoefu wake kazini.

“Nafasi yangu kama mkufunzi ni muhimu kwa sababu nawafunza wenzangu na kuwapa ujuzi unaohitajika kukabiliana na hali ngumu porini. Ninawafunza kuhusu sheria, huduma ya kwanza na jinsi ya kujihami ili kutekeleza wajibu wao vyema. Kabla nifuzu nilipitia mafunzo mengi ambapo kila mara nilifaulu,” alisema.

Bi Mwandaa alisema kuwa amepata changamoto nyingi kazini haswa kukabiliana na wawindaji haramu na shughuli nyingine haramu, kama vile ukataji wa miti ili kuchoma makaa.

“Sisi kama walinzi tuna mawasiliano ya moja kwa moja na jamii na hivyo inatulazimu kujitokeza haraka punde tupatapo ripoti za uvamizi wa wanyamapori mashambani. Mara nyingi huitwa usiku wa manane kuwatoa ndovu mashambani,” akasema.

“Ni lazima tuwe tayari kila wakati kwa kuwa hatujui kitakachotokea mbeleni. Wakati mwingine mashambulio hutokea wakati tunapopiga doria na hivyo kutulazimisha kukabiliana na wahalifu,” akasema.

Tangu ajiunge na kampuni ya Wildlife Works miaka 13 iliyopita amefungua njia kwa walinzi wa kike zaidi, ambapo leo, yeye ni mmoja wa wanawake kumi katika timu inayokua ya walinzi zaidi ya 100.

Ndoto yake ni kuwa siku zijazo kuwepo na wanawake wengi watakaojiunga katika uhifadhi haswa kazi ya ulinzi wa wanyamapori.

“Lengo langu ni kufikia wakati ambapo jinsia haitakuwa kikwazo cha kufaulu kwa ndoto za mtu. Mafanikio yangu sio tu ushindi wa kibinafsi bali ni hatua muhimu kwa wanawake wote katika uhifadhi. Nataka safari yangu iwahamasishe walinzi wa kike wanaotamani kuingia katika sekta hii. Kila mara nahimiza wanawake wafanye kazi kwa bidii na kufuata taaluma hii,” akasema.

Anasema kazi yake katika kampuni ya Wildlife Works sio tu kuhusu kulinda wanyamapori bali pia kuhusu kuleta mabadiliko ya uhifadhi ambapo vizazi vijavyo vinaweza kusaidika.