Habari Mseto

Mwanafunzi mwenye ndoto ya urubani aomba msaada wa karo

January 12th, 2024 2 min read

NA CECIL ODONGO

AKIWA ameubeba mfuko wenye stakabadhi ya matokeo yake ya Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE 2023), Michelle Atieno,12, anaingia kwenye boma la aliyekuwa mwalimu wake mkuu Bw John Obong’o katika wadi ya Kabonyo Kanyagwal, Kaunti ya Kisumu.

Akiwa na macho makavu, ishara kuwa alikuwa amelia sana, Michelle anampata Bw Obong’o ambaye anaugua na alistaafu miaka miwili iliyopita, akiwa ameketi chini ya mti na kuanza kumuelezea masaibu yake.

Dogo huyo aliitwa kujiunga na Shule ya Wasichana ya Asumbi inayopatikana Kaunti ya Homa Bay, lakini wanafunzi wa Kidato cha Kwanza watakapokuwa wakiripoti shuleni Januari 15, 2024, kwake hilo halitawezekana endapo mambo yatasalia jinsi yalivyo.

Mwanafunzi huyo alipata alama 392 akisomea katika Shule ya Msingi ya Kandaria iliyoko eneobunge la Nyando.

Hata hivyo, kwa sasa hajapata mdhamini na kipato kidogo cha familia hakiwezi kumsaidia kupata karo.

“Nilikuja kwa aliyekuwa mwalimu wangu mkuu ili nijadiliane naye kuhusu njia ambazo anaweza kunisaidia kupata elimu. Nafahamu ni mgonjwa pia. Nilitia bidii na kupata alama nzuri lakini babangu ana kiharusi naye mamangu anafanya vibarua tu kutukimu na hawezi kumudu karo yangu,” akasema Michelle.

“Msaada wangu utatoka wapi? Nawaomba wahisani wajitokeze wanisaidie kwa sababu ningependa kuwa rubani. Nilisoma kwa bidii na nataka kuinua maisha ya familia yetu ila hilo litafanyika tu  kama nitajiunga na Asumbi Girls na kuendelea na masomo yangu,”

“Naahidi nitatia bidii, tafadhali Wakenya nisaidieni nijiunge na Kidato cha Kwanza,” akasema msichana huyo mdogo akiwa amelemewa na hisia.

Babake Michelle, Bw Moses Odhiambo ambaye amekuwa na matatizo ya kiafya tangu apate kiharusi miaka michache iliyopita, amesema hana hanani. Bw Odhiambo anasema kuwa hana karo wala pesa za kumnunulia mwanawe mahitaji ya kuenda shuleni.

“Afya imenikataa. Sina furaha. Naomba msaada ili binti yangu ajiunge na Asumbi Girls. Huyu msichana ni mwerevu na nina kila imani atasaidia kuinua maisha ya familia hii kwa kupata elimu,” akasema.

Jumatatu inaendelea kukaribia na ombi la Michelle ni kuwa atapata mfadhili wa kumsaidia kujiunga na Asumbi Girls.

[email protected]