Habari Mseto

Mwanafunzi mwenye shabaha ya kuwa daktari aomba ufadhili

January 13th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

KIJANA Ndung’u Isaiah Njaramba kutoka Kaunti ya Murang’a sasa anaomba wahisani wamsaidie kujiunga na Shule ya Upili ya Njiiris alikoitwa baada ya kupata alama 310 katika Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) 2023.

Babake kijana huyo ndiye mlezi wake pamoja na ndugu zake wawili walio katika Gredi ya Tano.

Mzazi wake kijana huyo hana kipato cha kutosha kumuwezesha kulipa karo mwanawe aingie Kidato cha Kwanza.

Kijana huyo anahitaji jumla ya Sh20,535 za muhula wa kwanza ndipo akubaliwe shuleni kwa masomo.

Lakini pia atahitaji Sh15,000 za kununua vitu kama sare, godoro na vinginevyo vya kumfaa katika shule hiyo ya malazi ya kiwango cha kimkoa yaani extra-county.

“Hii ndiyo nafasi ya kipekee niliyo nayo ya kuanza safari yangu ya tiketi ya kuingia chuo kikuu ili nisomee udaktari nije niwe daktari wa upasuaji,” akasema kijana Isaiah.

Alisema hangetaka afungiwe nje katika nafasi hii ya kujiunga na shule ambayo hufanya vyema “na ambayo niliitwa kulingana na bidii yangu”.

Katika matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE 2023), shule hiyo ilifanikiwa kutuma wanafunzi 423 kati ya 526 waliofanya mtihani huo hadi vyuo vikuu baada ya kupata alama ya C+ kwenda juu.

Waliopata alama ya A walikuwa watatu, 45 wakapata A- huku wa B+ wakiwa 67.

Waliojipa alama ya B walikuwa 105, wa B- wakiwa 91, wa C+ wakawa 111. Waliopata C walikuwa 57 nao wa C- wakawa 33. Wa D+ walikuwa 12 huku wa D wakiwa wawili.

Kijana huyo alililia viongozi husika katika Kaunti hiyo wakiongozwa na gavana Irungu Kang’ata, Seneta Joe Nyutu, Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Murang’a Betty Maina, mbunge wa Kigumo Joseph Munyoro na diwani wa eneo hilo, Bw Boniface Mbau waingilie kati.

“Mimi naomba nisaidiwe kwa kuwa hakuna vile kwa sasa ambapo babangu kibarua anaweza akapata hizo Sh41,000 ambazo kwa mwaka mmoja zinahitajika,” akasema kijana huyo.

Babake naye alisema: “Nina imani kwamba atokea mtu wa kumsaidia kijana wangu asipoteze mkondo wake wa kuwa tegemeo katika familia hii.”

[email protected]