Habari za Kitaifa

Mwanahabari wa NMG Rukia Bulle kidedea Tuzo ya BBC ya Komla Dumor 2024

Na BENSON MATHEKA August 14th, 2024 2 min read

MWANAHABARI wa Nation Media Group Rukia Bulle ndiye mshindi wa 2024 wa Tuzo ya BBC ya Komla Dumor. Tangazo hilo limetolewa kwenye tovuti ya BBC Jumatano asubuhi.

Bi Bulle ni Mkenya wa tatu kushinda tuzo hiyo tangu kuanzishwa kwake 2015 kwa heshima ya marehemu mtangazaji wa Ghana na mwanahabari wa BBC Komla Dumor.

“Majaji walifurahishwa na ustadi wa Bi Rukia, uthabiti na uwezo wa kushughulikia hadithi zenye changamoto, umakini wake katika kuangazia watu wasio na uwakilishi na uwepo wake mkubwa,” ilisema BBC.

Bi Rukia ni ripota wa runinga ya NTV na ameangazia matukio mbalimbali ya kitaifa na habari kote nchini, akibobea katika hadithi zinazovutia watu. Pia huandikia www.nation.africa na Daily Nation.

Kama sehemu ya tuzo hiyo, Bi Rukia, 26, kwa muda wa miezi mitatu atafanya kazi na kikosi cha habari cha BBC kwenye televisheni, redio na mtandaoni jijini London, kupata uzoefu muhimu, ushauri na fursa nyinginezo. Pia atasafiri hadi nchi moja ya Kiafrika atakayochagua ili kuandaa habari ambayo itaonyeshwa kwenye BBC News.

Komla Dumor, anayejulikana kwa kusimulia hadithi na kujitolea kwake kuwakilisha na kuripoti kwa uhalisi masuala ya Kiafrika, alikuwa mwandishi wa habari aliyesifika sana ambaye alipeperusha makala ya Focus on Africa kwenye BBC World News. Aliaga dunia ghafla mnamo Januari 2014.

Aonea fahari ufanisi wa kutambuliwa kimataifa

“Kushinda tuzo hii ni jivunio kubwa sana kwangu. Nikiwa mwandishi wa habari, huwa ninajitahidi kila mara kufanya kazi kadri ya uwezo wangu, bila kujali kutambuliwa. Kwa hivyo, kutambuliwa kwenye jukwaa la kimataifa kupitia Tuzo ya Komla Dumor kumenitia moyo sana.

Nilitaka kuheshimu na kuchangia urithi wa Komla kwa namna fulani. Alikuwa mmoja wa waandishi wa habari bora wa kizazi chake; alionyesha sababu halisi ya  uandishi wa habari: ukweli, usahihi na usawa.

Tuzo hii itachochea shauku yangu na kunitia moyo niwe mwanahabari bora zaidi. Natumai tuzo hii itawatia moyo wasichana wachanga kama mimi, wanaovaa hijabu na kutoka jamii za walio wachache, kuwa na ndoto kubwa na kufikia malengo yao,” akasema Bi Rukia.

Bi Rukia ana shahada ya uandishi wa habari kutoka Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Amerika (USIU). Kwa sasa anasomea shahada ya uzamili katika Uhusiano wa Kimataifa katika chuo kikuu hicho.

“Hizi ni habari za kufurahisha kwetu kama jamii pana ya NMG. Kwa niaba ya kikosi cha watayarishi wa mada na vipindi wa NMG, natoa pongezi zangu za dhati kwa Rukia na kumtakia kila la heri anapoelekea London katika siku zijazo,” Joe Ageyo, Mhariri Mkuu wa NMG alisema.

Bi Rukia alitajwa mnamo 2023 kuwa miongoni mwa Waislamu 100 Wenye Ushawishi Zaidi nchini Kenya. Amejenga ufuasi mkubwa kwenye TikTok kupitia maudhui yake yanayoelimisha kuhusu maisha ya mwanahabari.

Wanahabari wengine wa Kenya waliowahi kushinda tuzo hiyo ni Wahiga Mwaura (2018), ambaye kwa sasa ni mtangazaji mkuu wa Focus on Africa na Victoria Rubadiri (2020)  ambaye kwa sasa anafanya kazi na CNN.