Habari Mseto

Mwanamke ashtakiwa kwa kulaghai vijana mamilioni kwa ahadi ya kazi

January 26th, 2024 2 min read

NA TITUS OMINDE

MWANAMKE wa umri wa miaka 60 ameshtakiwa kwa kujipatia pesa kwa njia za ulaghai kinyume na kifungu cha 313 cha Kanuni ya adhabu.

Bi Dinah Jepchumba alifikishwa mbele ya Hakimu Mkuu wa Eldoret Dennis Mikoyan na kushtakiwa kwa makosa 36.

Mahakama iliambiwa kwamba mshtakiwa alijipatia pesa hizo kutoka kwa vijana 36 wasio na kazi kwa ahadi ya kuwasaidia kupata nafasi za ajira katika jeshi la Uingereza.

Kila mmoja wa waathiriwa alilipa kati ya Sh40,000 hadi Sh150,000 kulingana na mpango na maelezo ya kazi lengwa.

Upande wa mashtaka uliambia mahakama kwamba mshtakiwa alijipatia fedha hizo kutoka kwa vijana wanaoishi katika mazingira magumu kwa tarehe tofauti kati ya Juni na Julai 2023.

Vijana hao walikuwa wameahidiwa kuanza kusafiri hadi Uingereza kabla ya Septemba 2023 lakini walianza kutilia shaka mpango huo mshtakiwa alipoanza kuwazungusha.

“Niliingiwa na mashaka kabla ya mwezi mmoja ili nisafiri Uingereza. Mshtakiwa kupitia wakala wake alipaswa kunilipia tiketi ya ndege kwa mujibu wa makubaliano yetu lakini alibadilika ghafla na kuanza kuniambia nijiandae kujilipia tiketi ya ndege kuenda Uingereza. Makubaliano yalieleza kuwa angenilipia safari baada ya kulipa ada iliyohitajika ya Sh150,000,” alisema mmoja wa waathiriwa.

Waathiriwa waliripoti kisa hicho katika kituo cha polisi cha Naiberi ambapo polisi walianzisha uchunguzi kuhusu madai yao.

Maafisa wa upelelezi kutoka kitengo cha DCI Eldoret Mashariki walisema kwa ripoti yao kwamba kuna mtandao wa kuwalaghai vijana mamilioni ya pesa kwa ahadi ya kuwasaidia kupata nafasi ya ajira katika jeshi la Uingereza.

Uchunguzi uliofanywa na maafisa wa upelelezi kutoka kituo cha polisi cha Naiberi hatimaye ulifanikisha kukamatwa kwa mshukiwa baada ya uchunguzi wa mwaka mmoja.

Hati ya mashtaka ilisema kuwa mshtakiwa pamoja na wengine ambao hawakufika mahakamani walipokea pesa hizo katika afisi yake iliyoko City Plaza mjini Eldoret kwa tarehe tofauti kati ya Juni na Julai 2023.

Mshtakiwa alikana mashtaka yote ambayo yamewasilishwa katika faili tatu za mahakama zilizosajiliwa kama E164, E187 na E188/2024.

Afisa wa upelelezi kupitia kwa wakili wa serikali Anthony Fedha alipinga kuachiliwa kwake kwa dhamana.

Akitoa ombi la kumnyima dhamana, Bw Fedha aliiambia mahakama kuwa mshtakiwa alikuwa hatarini na waathiriwa zaidi bado hawajaandikisha taarifa na kuhofia kwamba ikiwa mshtakiwa ataachiliwa kuna uwezekano wa kuingilia mashahidi wa upande wa mashtaka.

Mshtakiwa ambaye alionekana kuwa na wasiwasi kizimbani hakupinga kunyimwa dhamana.

Kesi hiyo itatajwa Januari 29, 2024, wakati mahakama itakapotoa uamuzi kuhusu ombi la dhamana.