Michezo

Mwanariadha Joshua Cheptegei wa Uganda avunja rekodi ya dunia katika mbio za mita 5,000

August 15th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

BINGWA wa dunia katika mbio za mita 10,000 Joshua Cheptegei wa Uganda, alitumia kivumbi cha Wanda Diamond League jijini Monaco, Ufaransa mnamo Agosti 14, 2020, kuvunja rekodi ya dunia iliyokuwa imedumu kwa kipindi cha miaka 16 kwenye mbio za mita 5,000.

Mwanariadha huyo mwenye umri wa miaka 23 alitawala mbio za mita 10,000 kwenye Riadha za Dunia zilizoandaliwa jijini Doha, Qatar mnamo 2019.

Cheptgei alikamilisha mbio za mita 5,000 kwenye Diamond League kwa muda wa dakika 12:35.36 na kuivunja rekodi ya dakika 12:37.35 iliyowekwa na Kenenisa Bekele wa Ethiopia mnamo 2004.

Ni mara ya pili kwa Cheptegei kuweka rekodi mpya ya dunia jijini Monaco msimu huu licha ya kalenda ya riadha za kimataifa kuvurugwa pakubwa na janga la corona.

Mtimkaji huyo alivunja tena rekodi ya mbio za kilomita tano zilizoandaliwa nchini Ufaransa mnamo Februari 2020.

Kwingineko, bingwa wa dunia katika mbio za mita 200, Noah Lyles aliendeleza ubabe wake katika fani hiyo jijini Monaco kwa kuweka muda wa sekunde 19.72. Kakaye mdogo, Josephus aliambulia nafasi ya pili mbele ya Mwingereza Adam Gemili aliyeandikisha muda wa sekunde 20.68.

Katarina Johnson-Thompson aliyeibuka bingwa wa dunia katika heptathlon nchini Qatar mwaka jana, alikiri kwamba hakuwa katika fomu nzuri ya kushindana jijini Monaco baada ya kurushwa hadi nafasi ya sita kwenye mashindano ya urukaji juu. Aliruka urefu wa mita 1.84, sentimita 14 chini ya rekodi aliyoweka 2019.

Mbali na Cheptegei, mwanariadha mwingine aliyeweka rekodi mpya kwenye mbio za Diamond League nchini Ufaransa, ni Mwingireza Laura Muir ambaye alivunja rekodi ya miaka 21 ya kitaifa iliyowekwa na Dame Kelly Holmes nchini Uingereza katika mbio za mita 1,000. Mbio hizo zilitawaliwa na Mkenya Faith Kipyegon. Muir aliandikisha muda wa dakika 2:30.82 katika mbio hizo.

Karsten Warholm wa Norway pia alivunja rekodi ya dunia Kevin Young katika mbio za mita 400 kuruka viunzi mnamo 1992 baada ya kufika utepeni kwa muda wa sekunde 47.10.

Bingwa wa dunia na mshindi mara tatu wa Diamond League, Timothy Cheruiyot alitawala mbio za mita 1,500 na kuwapiku Jakob Ingebrigtsen wa Norway na Jake Wightman wa Scotland aliyeibuka katika nafasi ya tatu kwa muda wa dakika 3:29.47.

Bingwa wa dunia na Jumuiya ya Madola katika mbio za mita 5,000 Hellen Obiri, alitetea taji lake la Diamond League nchini Ufaransa baada ya kumpiku Laura Weightman wa Uingereza. Bingwa wa dunia katika mbio za mita 10,000 na mita 1,500 Sifan Hassan wa Uholanzi aliyepigiwa upatu wa kumpiga kumbo Obiri, alishindwa kukamilisha mbio hizo za mita 5,000.