Habari za Kitaifa

Mwangaza ‘aenda’ na maji

Na CHARLES WASONGA August 21st, 2024 1 min read

GAVANA wa Meru Kawira Mwangaza amepoteza kiti chake baada ya maseneta kupitisha hoja ya kumtimua afisini iliyopitishwa na madiwani wa kaunti hiyo majuzi.

Jumla ya maseneta 26 walipiga kura ya NDIO, kuunga mkono shtaka la kwanza dhidi ya Bi Mwangaza – la ukiukaji wa Katiba na sheria nyinginezo.

Maseneta 4 walipiga kura ya LA kwa shtaka hilo, huku wengine 14 wakisusia upigaji kura.

Katika shtaka la pili la mienendo mibaya, maseneta 26 walipiga kura ya NDIO na kukubaliana na msimamo wa madiwani wa Kaunti ya Meru, 2 wakakatalia mbali shtaka hili huku 14 wakisusia kupiga kura.

Jumla ya maseneta 27 walikubaliana na hoja iliyopitishwa na Bunge la Kaunti ya Meru kwamba Bi Mwangaza alitumia vibaya mamlaka ya afisi yake, huku mmoja akipiga kura ya kumwondolea Mwangaza lawama.

Maseneta 14 walisusia upigaji kura kuhusu shtaka hilo.

Idadi kubwa ya maseneta waliosusia upigaji kura kuhusu mashtaka hayo matatu walikuwa ni wale wa mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya.

“Kwa mujibu wa Kipengele 181 cha Katiba na Sehemu ya 33 ya Sheria ya Serikali za Kaunti na Sheria za Seneti nambari 86, Seneti imeamua kumwondoa afisini Gavana wa Meru Kawira Mwangaza,” Spika wa Seneta Amason Kingi akasema kwenye uamuzi wa mwisho aliosoma mwendo wa saa tano za usiku, Jumanne, Agosti 20, 2024.

Awali, Bi Mwangaza alipinga mashtaka yote dhidi yake akishikilia kuwa hayakuwa na msingi wowote na yalichochewa na mahasidi wake wa kisiasa.

Bi Mwangaza sasa anashikilia rekodi kama Gavana wa Kwanza kuondolewa afisini baada ya uchaguzi mkuu wa 2022.

Hii ilikuwa mara ya tatu kwa madiwani wa Kaunti ya Meru kumtimua Bi Mwangaza.