Habari za Kaunti

Nani atategua kitendawili cha mashamba ya miwa kuteketezwa Kisumu?

Na VICTOR RABALLA September 12th, 2024 2 min read

WASIWASI umetanda kufuatia ongezeko la mioto ya kutatanisha ambayo imeteketeza ekari zaidi ya 1,000 za mashamba ya miwa katika Kaunti ya Kisumu.

Mioto hiyo ambayo imeathiri zaidi wadi za Miwani na Ombeyi vilevile imeharibu ekari 300 za mashamba yanayomilikiwa na kampuni ya sukari ya Kibos.

Msimamizi wa Huduma za Kilimo katika kampuni ya sukari ya Kibos , Richard Sewe, amesema visa hivyo vimeathiri zaidi shughuli zao za kila siku na michakato ya uzalishaji huku wakihangaika kushughulikia visa vya moto vinavyozidi kuongezeka.

‘Kufikia sasa, tuna tani 9,000 za miwa iliyochomeka ambayo bado haijavunwa,” alisema Bw Sewe.

“Tunalazimika kufanya kazi mchana na usiku ili kuokoa kile ambacho wakulima wametolea jasho kwa mwaka moja na nusu.”

Mioto hiyo iliyoanza Juni kufikia sasa imeharibu tani 36,000 ya thamani ya Sh180 milioni kulingana na bei ya sasa ya Sh5,000 kwa kila tani iliyoidhinishwa na mdhibiti wa sukari.

Kibos ambayo vilevile inajishughulisha na uundaji wa karatasi, pombe na uzalishaji wa umeme, ilisema haiwezi kutumia miwa iliyoungua kuendesha shughuli zake.

Miwa iliyokauka na kuungua inavuruga ubora wa bidhaa zetu,” alisema akitoa wito kwa mashirika ya usalama kufanya hima kudhibiti kero hilo.

Wakulima pia wanakabiliwa na tishio la kupata hasara kubwa kwa sababu miwa hiyo iliyokauka imepoteza uzani kwa kiasi kikubwa.

Kero hiyo imeshurutisha kampuni ya sukari ya Kibos kusitisha mpango wake wa kuvuna hali ambayo imesababisha miwa kukomaa kupita kiasi na mapato ya wakulima kudorora.

Msimamizi wa mawasiliano katika kampuni hiyo, Joyce Opondo, hata hivyo, ametaja suala hilo kuwa hujuma kutoka kwa washindani wao wanaotaka kulemaza shughuli zao.

“Haiwezi ikawa sadfa kwamba ni Kibos pekee inayoathiriwa,” alisema.

Bw Sylvanus Onyango ambaye shamba lake la miwa la ekari 44 liliteketezwa alisema alipoteza Sh7.9 milioni.

“Niliandikisha ripoti kuhusu suala hilo katika Kituo cha Polisi cha Nyangeta na afisi ya msimamizi eneo hili lakini wahusika bado hawajakamatwa,” alisema.

Wadi ya Miwani ndiyo imeathiriwa zaidi baada ya ekari 871 sawa na tani 28,232 kuteketezwa, takwimu za kaunti zinaonyesha.