Habari

Ndege yatoweka angani katika milima ya Aberdares

June 5th, 2018 1 min read

Na FAUSTINE NGILA

NDEGE moja ya humu nchini iliyokuwa imebeba watu kumi Jumanne jioni ilitoweka angani kilomita 60 kutoka jijini Nairobi, kamanda wa polisi katika Kaunti ya Trans Nzoia Samson Ole Kine alithibitisha.  Ilikuwa inatoka mjini Kitale ikielekea Nairobi.

Ndege hiyo aina ya Cesna C208 yenye nambari ya usajili 5YCAC inamilikiwa na kampuni ya humu nchini ya Fly Sax, na inakisiwa kutoweka kwa mawimbi ya udhibiti wa safari za ndege, rada, katika eneo la msitu wa Aberdares.

Shirika la Mamlaka ya Usimamizi wa Safari za ndege nchini (KCAA) lilithibitisha habari hizo kupitia akaunti yake ya Twitter Jumanne usiku.

“Tunathibitisha ripoti za ndege iliyokuwa ikitoka Kitale kuelekea Nairobi kutoweka angani. Ilionekana mara ya mwisho kwenye mawimbi ya rada saa nane na dakika mbili alasiri maili 40 kutoka jijini Nairobi ikipaa juu kwa urefu wa futi 11,000,” ukasema ujumbe.

Naibu Mkurugenzi wa Shirika la Huduma kwa Wanyamapori (KWS) anayesimamia maeneo ya milima, Simon Gitau Jumanne usiku alisema shughuli za kuitafuta ndege hiyo zimeanzishwa katika milima ya Aberdares.

“Utafutaji kwa njia ya angani hauwezekani kwa sasa kutokana na hali ya hewa lakini utafanyika Jumatano asubuhi,” akasema.

Habari zaidi kufuata…