• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 10:55 AM
Mtoto aaga dunia kwa kukosa kuhudumiwa hospitalini kwa saa tisa

Mtoto aaga dunia kwa kukosa kuhudumiwa hospitalini kwa saa tisa

NA LUCY MKANYIKA

FAMILIA moja katika eneo la Voi inalilia haki baada ya mtoto wa umri wa miaka minane kuaga dunia katika Hospitali ya Rufaa ya Moi katika Kaunti ya Taita Taveta, baada ya kusubiri matibabu kwa zaidi ya saa tisa.

Mtoto huyo ambaye alifariki mnamo Jumamosi alipangiwa kufanyiwa uchunguzi wa kichwa lakini afisa wa mashine ya CT Scan hakupatikana kwa kuwa hakuchukua simu.

Mvulana huyo ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi ya Mwanyambo mjini Voi, alikuwa akiugua saratani ya damu na alikuwa ametibiwa kwa muda wa mwaka mmoja katika Hospitali Kuu ya Kenyatta jijini Nairobi.

Kulingana na familia hiyo, mtoto huyo amekuwa akipata matibabu tangu Agosti 2022 hadi Agosti 2023 ambapo alishauriwa kutulia nyumbani na kuendelea kufanyiwa uchunguzi katika hospitali iliyo karibu naye.

Mamake Samuel Mwatate, Bi Euphemia Kinoi amesema kuwa huenda kifo cha mtoto wake kingezuiwa lau angepata matibabu kwa haraka.

Akiongea mjini Voi, Bi Kinoi alieleza jinsi walivyozungushwa katika hospitali hiyo na badala ya kupata usaidizi walipitia masaibu yaliyopelekea kifo cha mtoto wao.

“Nina uchungu sana kwa kuwa licha ya kutopokea matibabu maafisa wengine hawana utu. Wanafaa wawe na roho za kunitolea na kusaidia wanaotafuta matibabu katika hospitali hiyo,” alisema.

Babake mtoto huyo, Bw Scaver Nzai, alisema mwanawe alikuwa akipumzika nyumbani alipolamikia maumivu makali ya macho siku ya Ijumaa mchana.

Maumivu hao yalizidi hata baada ya kumpa dawa za kutuliza uchungu na hivyo kulazimika kumkimbiza katika hospitali hiyo kwa uchunguzi zaidi.

Daktari alipendekeza kwamba mvulana huyo alihitaji kipimo cha CT scan ili kujua sababu ya maumivu, lakini hakukuwa na afisa wa kufanya uchunguzi huo.

Bw Nzai alisema simu na jumbe kwa afisa huyo hazikujibiwa kuanzia saa kumi na moja jioni Ijumaa hadi saa 1.30 asubuhi Jumamosi wiki jana ambapo mtoto huyo alipofariki.

“Tulisubiri kwa saa nyingi bila msaada wowote. Nilipigia waziri wa Afya lakini hakunisaidia. Baada ya mwanangu kufariki nilimtumia ujumbe lakini hakunijibu. Mwanangu alikufa kifo cha kichungu sana,” alisema.

Bw Nzai alisema vilevile hakukuwa na oksijeni na wakalazimika kwenda kwa vyumba vya kulaza wagonjwa ili kuomba hewa hiyo ili waokoe maisha ya mtoto wao.

“Walituambia hakuna oksijeni hivyo tulikwenda wodini kuuliza kama kuna oksijeni kuokoa maisha yake. Tukapata moja kwenye wodi ya wanawake na tukaibeba na tukaipeleka kwa wauguzi ili iwekwe kwa mwanangu,” alisema.

Familia hiyo ilishutumu hospitali hiyo kwa kuzembea na kutaka uchunguzi ufanyike kuhusu suala hilo. Walisema wanataka hospitali hiyo iwajibike kwa kifo cha mtoto wao na kuhakikisha kuwa janga hilo halitokei tena.

“Tunataka haki kwa mtoto wetu. Hatutaki shida hii ipate mtu mwingine,” alisema Bw Nzai.

Alimtaka gavana na bunge la kaunti kuingilia kati na kuboresha hali katika hospitali hiyo. Alisema kuwa watu wengi katika kaunti hiyo wanategemea hospitali hiyo kwa mahitaji yao ya kiafya na kwamba wanastahili huduma bora.

Waziri wa Afya Bw Gifton Mkaya alisema uchunguzi wa kifo hicho unaendelea.

“Tutatoa ripoti ounde tu uchunguzi utakapokamilika,” alisema.

  • Tags

You can share this post!

Handisheki ya kisiri ilishafanyika kitambo, ni picha...

Amerika yaambia kampuni, raia wake wasianzishe biashara...

T L