Habari za KitaifaMakala

Ngilu akaidi Kalonzo akiomba eneo la ukambani liungane na serikali ya Kenya Kwanza


ALIYEKUWA Gavana wa Kitui Charity Ngilu ameiomba jamii ya Wakamba ikumbatie utawala wa Kenya Kwanza ili inufaikie miradi mbalimbali ya maendeleo kutoka sasa hadi mnamo 2027.

Bi Ngilu aliwataka viongozi wa sasa wa Ukambani kuiongoza jamii katika kuunga serikali kwa kufanya kazi na Rais William Ruto.

Alisema hii ndiyo njia pekee ya kunufaika kwa muda wa miaka mitatu inayokuja kabla ya kuamua mustakabali wao wa kisiasa 2027.

“Naomba Wakamba wajipange na kuunga utawala wa Rais Ruto kwa muda wa miaka mitatu ambayo imebaki. Lazima tuwe sehemu ya utawala wa sasa ili tunufaike kimaendeleo,” akasema Bi Ngilu.

Gavana huyo wa zamani wa Kitui alikuwa akiongea Jumamosi wakati wa mazishi ya Janet Kalekye Mutito, 82 wadi ya Mulango Kitui ya Kati. Aliwataka wakazi wa nyumbani kwake wawe kati ya watakaonufaika na miradi ya kuinua ufugaji na kupambana na ukame.

Kiongozi huyo wa Narc alishangaa kwa nini eneo hilo lilikuwa likiachwa nje ilhali Nyanza na Gusii zimeanza kuvuna miradi ya maendeleo licha ya kutompigia kura Rais Ruto mnamo 2022.

“Uamuzi wa Raila kufanya kazi na Ruto utafungua Nyanza kupitia kujengwa kwa reli ya kisasa ambayo itaunganisha Kisumu-Nairobi,” akasema Bi Ngilu.

Kiongozi huyo alisema Kitui ni kaunti ambayo inaweza kungáa kiuchumi kutokana na maliasili na ni kupitia ushirikiano na serikali, ambapo wakazi wengi watainuliwa kutoka lindi la umaskini.

Aliahidi kuwa ni kutokana na ushirikiano wa serikali ambapo kilimo cha unyunyuziaji mashamba maji, ufugaji, uchimbaji wa madini na utalii, utashamiri sana Kaunti ya Kitui.

Aidha aliwataka wanasiasa wa eneo hilo waweke kando tofauti zao kwa ajili ya maendeleo lakini wawashawishi raia wafanye kazi kwa karibu na serikali kwa ajili ya kutatua changamoto kadhaa zinazowaathiri.

Bi Ngilu alijiondoa katika kinyángányiro cha ugavana mnamo 2022 kwa ahadi kuwa angeteuliwa kwenye baraza la mawaziri iwapo Azimio ingeshinda kura hiyo.

Kiongozi huyo aliongeza kuwa ili mmoja wa viongozi wa Ukambani ashinde Urais, lazima wakazi wajitume na kutwaa vitambulisho kisha kujisajili kama wapigakura.

“Lazima tujitume ili kushinda Urais Lazima tutembee kutoka kijiji kimoja hadi kingine kuwashaajisha watu wetu wajisajili kama wapiga kura na pia wajitokeze siku ya kura,” akasema.

Kauli ya Bi Ngilu inaenda kinyume na Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka ambaye amekuwa akipinga hatua ya Kinara wa Azimio Raila Odinga kuanzisha ushirikiano na serikali ya Kenya Kwanza.

Bw Musyoka tayari amejitangaza kuwa kiongozi wa upinzani baada ya Bw Odinga kutangaza kuwa anawania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Kalonzo alisema hatua ya vigogo wa ODM kuteuliwa mawaziri ndani ya Kenya Kwanza ilikuwa usaliti mkubwa kwa upinzani na ulilenga sana kudhoofisha maandamano ya Gen Z ambayo yalikuwa yakiendelea nchini.

Tayari kiongozi wa DAP-K Eugene Wamalwa na Katibu Mkuu wa Jubilee Jeremiah Kioni wametangaza kuwa wanaunga mkono azma ya Bw Musyoka ya kuongoza upinzani wakisema ni mwanasiasa mwenye tajiriba pana na atajaza pengo la Bw Odinga.

Bi Ngilu amekuwa na historia ya kutofautiana kisiasa na Bw Musyoka na wawili hao wamekuwa pamoja katika kura za 2002, 2017 na 2022.

Bi Ngilu alihimili mawimbi makali ya kisiasa Ukambani na kuhudumu kama mbunge wa Kitui ya Kati mnamo 1992, 1997, 2002, 2007 japo akapoteza Useneta 2013 kisha kutwaa ugavana mnamo 2017.