Habari za Kaunti

Ng’ombe 900 wa mfugaji kutoka Kenya wazuiliwa Tanzania, yadai faini ya Sh4.7 milioni


MAAFISA wa serikali ya Tanzania wanazuilia ng’ombe 900 wa mfugaji Mkenya kutoka kijiji cha Rombo, Kaunti Ndogo ya Kajiado Kusini, Kaunti ya Kajiado kwa madai ya kupatikana katika taifa hilo jirani bila kibali.

Bw Saisa Lekimangusi, 47, alisema ng’ombe wake walikuwa wakisimamiwa na wachungaji walipokuwa wakipelekwa malishoni kutoka kaunti ya Kwale,  Jumatatu, Julai 29, 2024.

Hapo ndipo maafisa wa Mbuga za Kitaifa Tanzania (Tanapa) waliwazuiliwa ng’ombe hao kuwa kuingia katika eneo linalosimamiwa na asasi hiyo, bila idhini.

“Maafisa hao walidai wachungaji hao walilisha mifugo hao ndani ya mbuga hiyo ingawa awali nilikuwa nimewaarifu kwamba nitawahamisha ng’ombe hao. Walikuwa  mpakani sio ndani ya himaya ya Tanzania,” akasema Bw Lekimangusi.

Baba huyo wa watoto 11 aliambia Taifa Leo kwamba maafisa wa Tanapa waliekeza ng’ombe wake hadi eneo la Seme nchini Tanzania ambako sasa wanazuiliwa.

Inaripotiwa kwa maafisa hao wanadai faini ya Tsh105,000 (Sh5,250) kwa kila ng’ombe.

Hii inamaanisha kuwa Bw Lekimangusi anahitaji kulipa  Sh4.7 milioni,  kwa usimamizi wa Tanapa, ili kukomboa mifugo wake.

“Hii ni faini ghali zaidi na siwezi kuimudu. Sasa nimeachwa bila mifugo wowote. Serikali yetu iingilie kati na ielewane na serikali ya Tanzania kabla wapige ng’ombe wangu mnada,” akaomba

Naibu Chifu wa Kata Ndogo ya Olelai Daniel Parasiato Jumanne jioni aliambia Taifa Leo kwamba kisa hicho kimeripotiwa katika afisi ya Kamishna wa Kaunti ili hatua zifaazo zichukuliwe.

“Suala hilo ni nyeti na huenda likahitaji maafisa wa ngazi za juu zaidi wa serikali kuingilia kati,” akasema Bw Parasiato.

Mbunge wa Kajiado Kusini Samuel Parashina naye alisema viongozi kadhaa wamelivalia njuga suala hili na kupasha habari asasi husika huku wakisaka maridhiano.

“Ni tukio la kusikitisha. Tunataraji kwamba maafisa wa Tanzania wataachilia mifugo hao bila masharti kwa moyo wa ujirani mwema,” Mbunge huyo akaeleza.

Kumekuwa na mizozo kadhaa kati ya maafisa wa serikali ya Tanzania na Wakenya wanaoishi katika eneo hilo la mpaka haswa kuhusiana na madai ya wafugaji kulisha mifugo wao ndani ya himaya ya Tanzania bila kibali.

Aidha, mnamo Mei mwaka huu maafisa watano wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kutoka kituo cha polisi cha Buruburu Kenya,  walikamatwa nchini Tanzania kwa kuingia humo bila kibali walipokuwa wakiwafuata washukiwa wa wizi wa magari.

Baadaye waliachiliwa huru baada ya ujumbe wa maafisa wa usalama kutoka Kenya kuelewana na wenzao wa Tanzania.

Mnamo mwaka wa 2017, serikali ya Tanzania ilipiga mnada ng’ombe 1,300 mali ya wafugaji raia wa Kenya.

Wakati huo,  aliyekuwa Rais wa Tanzania,  John Magufuli,  alidai maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Kenya yalikuwa yakiharibiwa na mifugo kutoka Kenya.