Habari za Kitaifa

Ni sherehe kwa hoteli ya Ruto inapovuna kandarasi nyingi za Serikali

September 8th, 2024 2 min read

HOTELI ya Rais William Ruto ya Weston, imepokea kandarasi nyingi za serikali kuliko hoteli nyingine yoyote jijini tangu alipochukua uongozi Septemba 2022.

Hii ni kulingana na Tovuti ya Habari za Ununuzi wa Umma.

Idadi kubwa ya kandarasi za serikali zilizoorodheshwa ambazo Weston Hotel imepokea ni baada ya Dkt Ruto kuingia mamlakani.

Hoteli hiyo, ambayo iko kando ya Barabara ya Lang’ata Nairobi, kufikia sasa imehusishwa na zabuni 37 za kusambaza bidhaa na huduma mbalimbali ya serikali za thamani ya Sh57.9 milioni ikiwemo kuandaa hafla za wizara, idara na serikali za kaunti.

Hii ni zaidi ya hoteli zingine jijini Nairobi zinazotoa huduma sawa na mikutano, kulingana na habari rasmi zinazopatikana kwa sasa.

Tovuti hiyo inaonyesha kwamba ni kandarasi sita pekee za thamani ya jumla ya Sh1,011,000 ambazo hoteli hiyo ilishinda kutoka kwa mashirika yanayohusiana na Serikali kabla ya Septemba 2022.

Hata hivyo, uchunguzi haujakamilika kwani baadhi ya wasambazaji na mashirika bado hayajaongeza maelezo yao kwenye tovuti kama inavyohitajika.

Maelezo zaidi yanayohitajika sasa kwa majarida yanayopatikana hadharani ni pamoja na orodha ya wenyehisa na wakurugenzi – kama sehemu ya hitaji la mpango wa ufadhili ambao Kenya imekubaliana na Shirika la Fedha Ulimwenguni (IMF).

Sehemu kubwa ya pesa ambazo Weston Hotel ilipokea zilitoka kwa Mamlaka ya ICT, ambayo ililipa Sh43.2 milioni kwa kutoa huduma za upishi wakati wa Mkutano wa Connected Africa kwa mwezi mmoja kuanzia Aprili 12 hadi Mei 13 2024.

Mkutano wa Connected Africa 2024, ulifunguliwa rasmi na Rais William Ruto eneo la Uhuru Gardens, Nairobi.

Kando na Rais William Ruto, wakurugenzi wengine walioorodheshwa wa Weston Hotel ni Bi Chebet Rael Kimeto (Bi Rachel Ruto) ambaye ni Mkewe Rais, na bintiye, Bi Sharlene Chelagat Ruto.

Hapo awali, Rais Ruto alikiri hadharani kumiliki hoteli hiyo huku maelezo yakichapishwa kwenye tovuti ya ununuzi yakithibitisha anahusika nayo.

Weston imepokea kandarasi nyingi zaidi kuliko hoteli zingine jijini Nairobi, huku Fairview ikiikaribia kwa kupata kandarasi 15.

Hilton Garden iliyoko barabara ya Mombasa, ambayo inapendwa na wabunge kwa mikutano yao ya kamati, pia imepata kandarasi kadhaa.

Uchunguzi huo wa umma unaonyesha kuwa Bunge la Kaunti ya Machakos imekuwa mteja mkuu wa Weston, kwa kuipa hoteli hiyo kandarasi 21.

Mashirika mengine ya serikali ambayo yameipa hoteli hiyo kandarasi ni pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Matibabu ya Kenya ambayo ina kandarasi 11 na Mamlaka ya Uwekezaji nchini, kandarasi tatu.