Habari za Kitaifa

Kuria : Niko na hisa Kenya Kwanza, siendi popote

August 18th, 2024 2 min read

ALIYEKUWA Waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria anaendelea kuteta baada ya kutemwa kutoka baraza la mawaziri.

Bw Kuria anaendelea kuwakejeli mawaziri wapya walioteuliwa na kula kiapa akiashiria kuwa watahitaji miujiza kutatoa huduma bora kwa Wakenya.

Mbunge huyu wa awali wa Gatundu Kusini alizungumza alipokuwa kaunti ya Nandi. Wakati uo huo RAIS William Ruto akizindua mradi wa maji wa zaidi ya Sh340 milioni katika eno la Nandi Hills.

Bw Kuria ambaye alikuwa akizungumza katika eneo la Kobujoi alisema ‘hana uchungu’ kwa kupoteza kazi yake kama waziri lakini alikaribisha hatua hiyo akisema kuwa Wakenya wote wana haki ya kupewa fursa ya kuwahudumia wananchi.

Tuliteseka kusaidia Ruto

Hata hivyo, Bw Kuria alisema wanasiasa kutoka Mlima Kenya waliteseka sana walipokuwa wakimfanyia kampeni Rais William Ruto  na hivyo basi wanastahili heshima na kutambuliwa kama wenye hisa kubwa serikalini kuliko sehemu nyingine yoyote ya nchi.

 “Wengi wetu kutoka Mlima Kenya ndio wanasiasa waliodhulumiwa zaidi tulipokuwa tukimpigia kampeni Rais Ruto, hivyo basi tunamiliki hisa kubwa za serikali hii,” alisema Bw Kuria.

Bw Kuria alisema kama wanahisa katika serikali ya Kenya Kwanza hawana mpango wa kugura serikalini licha ya kutimuliwa kama waziri akisisitiza kwamba hataondoka serikalini kwa vile ‘ana hisa’ katika utawala wa Rais Ruto.

Takriban mwezi mmoja baada ya kuvuliwa wadhifa wake wa uwaziri, Bw Kuria anaonekana kuungana na Naibu Rais Rigathi Gachagua kukariri siasa za hisa.

“Katika serikali hii ya William Ruto, sisi watu wa mlimani tuliteseka sana tukipigania Rais Ruto na wacha niwaambie kitu hatuendi popote, ukitufukuza kupitia mlango tunaingia kupitia dirishani, ukitufukuza kupitia kwa dirisha tunaingia kupitia kwa bomba la moshi, tuko hapa serikalini, hatuendi popote,” alisema Bw Kuria

Bw Kuria alionya kuwa iwapo watalazimika kutoka nje ya serikali kama wanahisa watadai mgao wao.

Kwa upande wake Dkt Ruto alisema mradi wa Usambazaji wa Maji Nandi Hills unapanuliwa ili kuongeza idadi ya familia zinazonufaika kutoka 1,000 hadi zaidi ya 10,000.

Alisema mradi huo utanufaika na Sh200 milioni kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika na kiasi kilichobaki kutoka kwa serikali.

“Tumejitolea kuhakikisha kuwa Wakenya kote nchini wanapata maji safi ya kunywa,” alisema Dkt Ruto.

Rais Ruto alimuagiza Waziri mpya wa Maji Eric Mugaa kuhakikisha kuwa walengwa wote 10,000 watasambaziwa maji kutoka kwa mradi huo katika muda wa miezi mitano ijayo.