Habari za Kitaifa

NTSA, IRA hawajui mahasla wanalipia bodaboda za mikopo

May 16th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

MAJINA ya wahudumu wa bodaboda huwa hayako kwenye stakabadhi za umiliki wa pikipiki wanazonunua kwa mikopo kutoka kwa kampuni mbalimbali zinazoendesha biashara ya kuuza vyombo hivyo vya uchukuzi nchini.

Haya yamefichuliwa Alhamisi na maafisa wakuu wa Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA) na Mamlaka ya Kusimamia Sekta ya Bima Nchini (IRA).

Maafisa wa asasi hizo walifika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Fedha kutoa maelezo kuhusu sakata ya kutwaliwa au kuibiwa kwa pikipiki zikiwa zinasalia na muda mfupi kabla ya wahudumu wa bodaboda kumaliza kuzilipia.

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Fedha Kuria Kimani akiongoza kikao cha kuchunguza sakata kuhusu ununuzi na wizi wa bodaboda za mikopo. PICHA | CHARLES WASONGA

Mkurugenzi wa utoaji leseni katika NTSA Aden Maalim, aliiambia kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Molo Bw Kuria Kimani kwamba majina ya wanabodaboda huwa hayapo katika stakabadhi zozote za mamlaka ndani ya kipindi cha malipo.

“Kama NTSA huwa hatuna majina au maelezo wa wanunuzi wa pikipiki hizi za mikopo bali yale ya wauzaji pekee. Ni baada ya wanunuzi hao kukamilisha malipo ndipo wao na wanunuzi huja kwetu ili tuhamishe umiliki kutoka kwa wauzaji hadi wananunuzi,” akasema Bw Maalim.

Bw Aden Maalim, afisa wa NTSA aliyefika mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Fedha mnamo Mei 16, 2024, katika jumba la Bunge Towers kutoa maelezo kuhusu sakata ya uuzaji na kuibiwa kwa pikipiki za mikopo. PICHA | CHARLES WASONGA

Aliwaeleza wabunge hao kwamba pikipiki hizo zinapopotea au kuibiwa, NTSA hushughulika na kampuni zilizoziuza wala sio wahudumu wa bodaboda.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Kutetea Wateja katika IRA Bi Monica Thirima alisema japo wahudumu wa bodaboda ndio hulipa bima kwa pikipiki hizo, fidia hulipwa kwa kampuni za kuziuza wala sio wahudumu hao.

“Wahudumu wa bodaboda hulipa kati ya Sh15,000 na Sh17,000 kama ada ya bima kwa pikipiki hizo. Lakini zikipotea, zile kampuni zilizoziuza ndizo hufidiwa kwa sababu wanabodaboda hao huwa hawatambuliwi kama wamiliki wa vyombo hivyo,” akasema Bi Thirima.

Kamati hiyo imekuwa ikichunguza kampuni tano za kuuza pikipiki kwa mikopo kuhusiana na sakata ambapo pikipiki hutwaliwa au huibiwa siku chache kabla ya wanabodaboda kumaliza kuzilipia.

Kampuni hizo ni Watu Credit Ltd, Mogo Motorcyle Kenya, JoyInc Group, 15 Minutes na My Boda.

Hii ni baada ya wanabodaboda kulalamika kuwa hulipia pikipiki hizo hadi Sh571,000 lakini baadaye kuibiwa kwa njia ya kutatanisha.