Habari za Kitaifa

Nyong’o aanza kuvaa viatu vya Raila kuongoza ODM


CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) kimemteua Gavana wa Kisumu, Prof Peter Anyang’ Nyong’o, kuwa kaimu kiongozi wake kufuatia kujiondoa kwa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga ambaye anazamia kampeni yake za uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).

Kamati Kuu ya Usimamizi ya Chama hicho (CMC) iliyoongozwa na Bw Odinga Jumatano ilimteua Prof Nyong’o, ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa ODM, kuongoza chama wakati waziri mkuu huyo wa zamani anazingatia kampeni za AUC.

‘Kwa kuzingatia ratiba ya kampeni ya kiongozi wa chama chetu na haja yake kufanya hivyo, amemteua Mheshimiwa Peter Anyang Nyong’o, Gavana wa Kisumu, kuongoza mikutano yoyote na ya Kamati Kuu ambayo inaweza kuwa muhimu wakati wa kutokuwepo kwake,” Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alitangaza baada ya mkutano huo uliofanyika katika Hoteli ya Nairobi.

Prof Nyong’o alikuwa miongoni mwa watu watano ambao majina yao yalitajwa kuongoza chama hicho baada ya Bw Odinga kuondoka.

Wengine walikuwa Magavana James Orengo (Siaya), Gladys Wanga (Homa Bay) – ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kitaifa wa ODM, Simba Arati (Kisii) – naibu kiongozi wa chama cha ODM pamoja na seneta wa Nairobi Bw Sifuna.

Afisa wa ndani katika ODM aliambia Taifa Leo baada ya mkutano wa Jumatano kwamba Prof Nyong’o alipata wadhifa huo “kutokana na tajriba yake katika chama na uaminifu mkubwa tangu kilipoanzishwa 2005.”

‘Kama katibu mkuu mwanzilishi, Prof Nyong’o ana kumbukumbu ya kitaasisi ya chama na tuna imani atakiongoza kufikia mafanikio zaidi,’ afisa huyo alisema.

Prof Nyong’o alikuwa miongoni mwa wanachama waanzilishi wa ODM, ambacho kiliundwa na watu waliopinga katiba iliyopendekezwa katika kura ya maamuzi ya 2005.

Baadaye kilibadilika kuwa vuguvugu la kisiasa na chama na kusajiliwa mnamo 2007.

Akiwa mmoja wa viongozi wakuu katika chama, Prof Nyong’o anatambuliwa kwa kukisaidia kuunda sera na mikakati yake.

Gavana huyo wa Kisumu amekuwa mshirika wa karibu wa Bw Odinga, akihudumu kama mshauri wake wa kutegemewa wakati wa kampeni kadhaa za urais na hata aliteuliwa kuwa kiongozi wa chama mwaka wa 2014 wakati Waziri Mkuu huyo wa zamani alipofanya ziara ya mwezi mmoja nchini Amerika.

“Amesalia kuwa mtetezi wa demokrasia ya kijamii, ambayo ndiyo itikadi ya kisiasa ya ODM. Ametekeleza jukumu kubwa ndani ya ODM, kama mwanachama mwanzilishi, kiongozi wa chama, mtaalamu wa mikakati, na kiongozi wa kaunti. Mchango wake ndani ya ODM unaonyesha kujitolea kwake kwa ukuaji wa chama na dhamira yake kuu katika siasa za Kenya. Afisa mmoja wa ODM alifichua kuwa Prof Nyong’o alipata wadhifa huo kwa vile ‘kulikuwa na hisia kwamba angeleta watu pamoja badala ya kuwatawanya.’

Prof Nyong’o alipongeza chama hicho kwa kumkabidhi jukumu hilo.

“Natoa shukrani zangu za dhati kwa kiongozi wetu, Mheshimiwa Raila Odinga na Kamati Kuu ya Usimamizi ya Chama cha ODM kwa kunikabidhi jukumu la Kaimu Kiongozi wa Chama. Ninathamini sana imani mliyoniwekea ya kusimamia chama huku Baba akihudhuria majukumu yake ya kimataifa,” Gavana huyo wa Kisumu alisema.

“Kwa familia nzima ya ODM kote nchini, ninawahakikishia kuwa tutaendelea kufuata nyayo za Baba tunapoinua chama chetu hadi viwango vya juu zaidi. Chama kiko imara,” aliongeza.