Michezo

Onana wa Manchester United atasaidia Cameroon katika Afcon?

January 9th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

GOZI la kutafuta bingwa wa soka katika bara la Afrika (Afcon) litaanza kusakatwa rasmi mnamo Januari 13 hadi Februari 11, 2024, nchini Cote d’Ivoire.

Kwa muda huo, klabu zinazoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) zitakosa wachezaji tegemeo.

Arsenal itakuwa inawakilishwa na Mohammed Elneny ambaye atakuwa akiwajibikia Misri.

Liverpool itampoteza kwa muda Mohammed Salah ambaye pia ni raia wa Misri.

Chelsea itakosa huduma za Nicolas Jackson ambaye ameitwa kuwajibikia Senegal.

Klabu ya Manchester United itakuwa haina huduma za nyani Andre Onana ambaye atakuwa akinyakia Cameroon katika kipute hicho cha Afcon. Pia, mashetani hao wekundu watakosa huduma za Sofyan Amrabat ambaye atafika kuwajibikia Morocco.

Tottenham itakuwa na pengo la mastaa Pape Matar Sarr atakayekuwa akiwikia Senegal huku naye Yves Bissouma akikimbia kuwajibikia taifa la Mali.

Aston Villa itamkosa Bertrand Traore ambaye ameitwa kwa majukumu muhimu nyumbani Burkina Faso.

Bournemouth itakuwa bila huduma za Dango Ouattara wa Burkina Faso na pia Antoine Semenyo wa Ghana.

Brentford itaaga kwa muda vifaa Yoane Wissa (DR Congo) na Frank Onyeka ambaye husakatia Nigeria.

Simon Adingra wa Ivory Coast atatua kwao kwa muda kutoka Brighton & Hove Albion huku Crystal Palace ikibakia kumkosa kifaa Jordan Ayew atakayefika kuulizia taifa lake la Ghana. Everton itakuwa bila huduma za Idrissa Gueye ambaye amefika kuwajibikia Senegal.

Timu ya Fulham itawakosa Fodo Ballo-Toure (Senegal), Calvin Bassey na pia Alex Iwobi wa Nigeria.

Luton Town itakosa Issa Kabore wa Burkina Faso huku Nottingham Forest ikikosa huduma za Serge Aurier ambaye ndiye nahodha wa Cote d’Ivoire na wenzake Willy Boly na Ibrahim Sangare, Moussa Niakhate na mwenzake Cheikhou Kouyate wa Senegal na pia Ola Aina wa Nigeria.

West Ham itawapoteza kwa muda Nayef Aguerd wa Morocco na Mohammed Kudus akihemea Ghana.

Sheffield United itawapoteza katika kipindi hicho Anis Ben Slimane wa Tunisia na Yasser Larouci wa Algeria huku Wolves ikikosa huduma za Rayan Ait-Nouri wa Algeria na Boubacar Traore wa Mali.

[email protected]