Michezo

Ongare kupiga ndondi za kulipwa katika kikosi cha ughaibuni baada ya Olimpiki za Tokyo, Japan

October 11th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

LICHA ya kuwa mwanamke wa kwanza raia wa Kenya kuwahi kujitwalia nishani kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola, Christine Ongare bado hajafichua mustakabali wake kwenye ulingo wa ndondi na amefichua azma ya kufanya hivyo baada ya Olimpiki.

Ongare aliduwaza wengi kwa kujinyakulia medali ya shaba kwenye mashindano ya Jumuiya ya Madola jijini Gold Coast, Australia mnamo 2018 na akapata umaarufu zaidi alipojikatia tiketi ya kushiriki mapambano ya Tokyo, Japan yaliyoashirishwa kutoka 2020 hadi 2021 kwa sababu ya corona.

“Nimepania kushughulikia kila kitu kwa wakati wake. Hivyo, Mungu akijalia, huenda nikaanza kuwazia kushiriki masumbwi ya kulipwa ughaibuni baada ya Olimpiki za Tokyo. Kwa sasa nawazia tu jinsi ya kujizolea medali katika mapambano hayo,” akatanguliza Ongare.

“Nataka kuwa Mkenya wa pili kuwahi kujishindia nishani ya dhahabu kwenye Olimpiki baada ya Robert Wangila mnamo 1988 jijini Seoul, Korea Kusini,” akasema.

Licha ya kwamba Olimpiki za Tokyo ziliahirishwa na kuratibiwa upya mwakani, Ongare amesisitiza kwamba hana presha ya kuingia katika sajili ya kikosi chochote cha ughaibuni kwa minajili ya kushiriki ndondi za kulipwa kwa wakati huu.

“Napania kujifua vyema zaidi kwa mashindano hayo yajayo kabla ya kuamua cha kufanya. Naamini zaidi katika kufanya mambo jinsi yajavyo, hatua kwa hatua,” akasema.

Kwa mujibu wa Kamati ya Kimataifa ya Olimpiki (IOC), michezo ya Japan iliyoahirishwa mwaka huu wa 2020 sasa itaandaliwa Julai 23, 2021 jijini Tokyo.

Ongare kwa sasa hujifanyia mazoezi katika ukumbi wa Avefitness, eneo la Lavington, Nairobi na analenga kupata kikosi cha humu nchini kitakachomshiriki kwenye mazoezi ya haiba kubwa zaidi kadri anavyolenga kunogesha Olimpiki za Tokyo.

“Nimekuwa nikitegemea maagizo ninayopokezwa na kocha wangu Benjamin Musa kupitia simu wakati huu wa janga la corona. Hivyo, ni vigumu sana kutathmini kiwango cha kuimarika kwa mtu,” akasema Ongare.

Ongare alijikatia tiketi ya Olimpiki kwa kumdengua Catherine Nanziri wa Uganda kwenye mchujo wa uzani wa flyweight (kilo 51) jijini Dakar, Senegal.

Idadi ya washiriki wa kiume kwenye uzani wa flyweight katika Olimpiki za Tokyo, Japan ilipunguzwa kutoka 10 hadi wanane huku ile ya wanawake ikiongezwa kutoka watatu hadi watano. IOC ilithibitisha uzani wa washiriki wa kila kitengo kwa minajili ya mashindano ya Tokyo, Japan mnamo Juni 19, 2019.