Makala

Polisi mstaafu mwenye umri wa miaka 102 bado anasoma Taifa Leo

April 1st, 2024 2 min read

NA BENSON MATHEKA 

ALISTAAFU mwaka wa 1964, mwaka mmoja tu baada ya Kenya kupata uhuru.

Na sasa akiwa na umri wa miaka 102, Koplo wa Polisi (Mstaafu) Peter Kivuva bado anapenda kusoma Gazeti lake analolipenda la Kiswahili, Taifa Leo.

Wanawe huhakikisha kwamba anapata nakala ya gazeti lake la kila siku la Taifa Leo kutoka mji wa karibu wa Tala katika Kaunti ya Machakos.

Lakini si mapenzi tu ya kusoma magazeti yanayomsisimua Mzee Kivuva, ana shauku ya elimu.

Kivuva anasema elimu ni zawadi bora ambayo wazazi wanaweza kuwapa watoto wao katika maisha yao.

Mzee Kivuva ambaye ni baba wa watoto kumi alizungumzia jinsi alivyokuwa akitumia pensheni yake ya kila mwezi ya Sh101 kukidhi mahitaji ya kimsingi ya familia, ikiwamo elimu ya watoto.

“Nilistaafu kazi ya polisi mwaka 1964 watoto wangu wote wakiwa sekondari na nilitumia pensheni hiyo kidogo kuhakikisha wanamaliza shule,” alisema mzee huyo.

Koplo wa Polisi (Mstaafu) Peter Kivuva, ambaye ni msomaji hodari wa Gazeti la Taifa Leo akilishwa keki wakati wa maadhimisho yake ya miaka 102. PICHA|BENSON MATHEKA

Alikuwa akizungumza na wanahabari nyumbani kwake kijiji cha Katine katika Kaunti ndogo ya Matungulu, wakati wa sherehe ya kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa aliyotimiza miaka 102 iliyohudhuriwa na watu wa karibu wa familia yake na zaidi ya majirani 600.

Alisimulia jinsi alivyoweza kutumia pensheni yake ndogo kusomesha watoto wake hadi viwango ambavyo kila mmoja angeweza kufikia.

Mzee Kivuva msomaji shupavu wa Gazeti la kipekee la Kiswahili Kenya – Taifa Leo, alihusisha umri wake na maombi, kujiamini na mazoezi.

Muumini dhabiti wa Kanisa la Jeshi la Wokovu, Mzee Kivuva alisema hakuna kitu kama ‘fedha ndogo’, akiongeza, mtu anahitaji usimamizi mzuri wa fedha.

Alisisitiza kuwa mtu anafaa kutengeneza maisha kwani hakuna kinachopatikana kwa urahisi.

Askari polisi huyo mstaafu alitumia fursa hiyo kuwaaga waumini wenzake wa kanisa hilo kutokana na umri wake mkubwa.

Mmoja wa wajukuu zake, Alfred Mutua, alimsifu babu yake kwa kulea familia yake vyema.

Mutua alisema kila mara wanahakikisha wako karibu na Mzee Kivuva na kwamba wanampeleka kanisani siku za Jumapili na pia katika baadhi ya gwaride za kawaida za barabarani.

Mwana wa tano wa Mzee Kivuva, John Kivuva, aliomba watoto kutunza sana wazazi wao wakizeeka.