Makala

Polisi walaumiwa majambazi wakivamia kampuni ya dhahabu mara sita Siaya

Na KNA September 10th, 2024 1 min read

NI mara ya sita mwaka huu kampuni ya dhahabu ya Amlight  Resources iliyoko Siaya imevamiwa na majambazi na kupoteza mali ya mamilioni ya pesa.

Na sasa, ndani ya majuma mawili yaliyopita, kampuni hiyo ya kuchimba madini kaunti ndogo ya Rarieda, imevamiwa mara mbili.

Sawa na matukio hayo mengine ya awali, shirika hilo limeendelea kupoteza mali ya mamilioni ya pesa.

Hivi punde

Katika tukio la hivi punde zaidi kijijini Ramba, Kata ya Asembo Central, usiku wa kuamkia Jumatatu, wezi hao walimfunga askari kwa kamba saa saba usiku kabla ya kusababisha uharibifu na wizi.

Waliteketeza tingatinga mbili.

Wakili Danstan Omari alilalama kuwa hili ni tukio la sita kufanyika mwaka huu na hakuna hatua imechukuliwa na vyombo vya usalama.

Bw Omari alizidi kuteta kuwa hata kesi walizowasilisha kortini zimekwama na kuganda.

Wakili huyu, ambaye alisema maisha yake yako hatarini, alisema amekuwa akifuatwa na watu  kwa nia ya kumtisha asiwakilishe kampuni hiyo katika shoroba za mahakama.

“Polisi na idara ya mahakama inaonekana kama imekula njama ili kuvuruga mchakato wa kutekeleza haki,” alilalamika wakili Omari akiongeza kwamba watataka kesi zote zinazosubiri kuwasilishwa mahakamani – zinazohusu Amlight Resources – zihamishwe nje ya kaunti ya Siaya ambako, alidai, mifumo ya mahakama imeingiliwa.

Alisema kuwa wanafikiria kushtaki polisi kwa kukataa kulinda mali ya kampuni hiyo licha ya maombi kadhaa yakitolewa.

Mkurugenzi wa kampuni ya Amlight Resources; Amos Mabonga aliunga mkono kauli ya wakili wake akilaumu mahakama na polisi kwa masaibu yanayoathiri kampuni yake.

Bw Mabonga alisema washindani wake wamewatuma majambazi ambao wamekuwa wakimfuata, na kuongeza kuwa ameweza tu kuishi kwa neema ya Mungu.

Wiki mbili zilizopita majambazi waliokuwa na silaha walivamia kampuni hiyo na kuondoka na vifaa vya thamani ya mamilioni ya pesa baada ya kuvunja ukuta na kuvunja afisi na karakana.

Imetafsiriwa na Labaan Shabaan