Habari

Raila apuuza madai waliongea na Ruto kabla ya handisheki

January 25th, 2020 2 min read

MOHAMED AHMED na BENSON MATHEKA

KINARA wa ODM Raila Odinga jana alipuuliza mbali madai kuwa alimfuata Naibu wa Rais William Ruto, akitaka waridhiane kabla ya handisheki yake na Rais Uhuru Kenyatta.

Bw Odinga alisema kuwa mazungumzo ya handisheki ambayo yamezaa ripoti ya BBI yalikuwa kati yake na Rais Kenyatta pekee na hakuna yeyote aliyehusika.

Akihojiwa na runinga ya NTV Alhamisi usiku, Bw Ruto alisisitiza kuwa Bw Odinga aliwasiliana naye kwanza kabla ya kuzungumza na Rais Kenyatta.

Hata hivyo, akiwa Mombasa jana, Bw Odinga alisema matamshi hayo ni ya kupotosha Wakenya.

“Jana niliona kuna mtu anadai kuwa nilimfuata. Mimi sikufuata mtu. Yalikuwa makubaliano kati yangu na Rais Kenyatta,” akasema Bw Odinga kujibu matamshi ya Bw Ruto.

Wakati huo huo, Bw Odinga alipinga madai kuwa anatumia BBI kujipangia mpango wake wa kuwania urais mwaka wa 2022 ama kumtafutia Rais Kenyatta nafasi ya waziri mkuu.

Akizungumza katika mkutano na viongozi wa eneo la Pwani kupanga mkutano wa kesho, Bw Odinga alisema kuwa madai hayo ni propaganda ambazo hazifai kusikilizwa.

“Hatujaleta BBI ili nipate kuwa rais ama Uhuru awe waziri mkuu. Msisikize hizo propaganda. Maono yetu kuhusiana na BBI ni kulenga kuunganisha Wakenya na kuwa na maongezi ya taifa zima,” akasema Bw Odinga.

Mnamo Jumatano akiwa Nairobi, Bw Odinga aliwataka Wakenya kupuuza madai ya Naibu Rais William Ruto na wandani wake wa kisiasa kwamba mchakato huo ni wa kumuandaa kugombea urais.

“Puuzeni wanaopotosha watu. Sijawahi kutangaza kwamba nina azma ya kugombea urais. Ripoti ya BBI haizungumzii masuala ya 2022. Hii ni ajenda ya kuunganisha Wakenya na inaendeshwa na Wakenya wenyewe,” alieleza Bw Odinga.

Alisema nia ya wanaodai kwamba BBI ni kuhusu uchaguzi mkuu wa 2022 ni kuwapotosha Wakenya.

“Wakenya wote wanakaribishwa kuwa sehemu ya mchakato huu. Wafahamu kuwa hakuna nguvu au hujma zinazoweza kusimamisha BBI,” alisema alipokutana na baadhi ya viongozi.

Ijumaa, Bw Odinga aliwaeleza maelfu waliohudhuria mkutano huo namna handisheki ilivyofikiwa na kuwahimiza kuichukulia kwa uzito ili kuwezesha kutatuliwa kwa masuala yanayoathiri eneo la Pwani.

Bw Odinga ambaye alikuwa ameandamana na magavana watano wa Pwani akiwemo Hassan Joho (Mombasa), Amason Kingi (Kilifi), Dhadho Godhana (Tana River), Fahim Twaha (Lamu) na Granton Samboja wa Taita Taveta, aliwahimiza wakazi hao wa Pwani kuhusu kuafikiana masuala ambayo wanataka yatatuliwe.

Alizungumza hayo na kutangaza kubadilishwa kwa sehemu ambayo mkutano huo utafanyika.

Bw Odinga alisema jana kuwa mkutano huo utafanyika katika bustani ya Mama Ngina Waterfront baada ya kutathmini kuwa uwanja wa Tononoka hautatosha kuhimili maelfu ya watu watakaojitokeza kesho.

“Tayari nimeongea na Rais pamoja na Waziri Balala na wamekubali tutumie eneo la Mama Ngina kwa ajili ya mkutano wetu,” akasema Bw Odinga.

Bw Joho kwa upande wake alisema kuwa walihofia kuwa huenda kukatokea mkanyagano eneo la Tononoka kwa sababu ya wale watu ambao wamepanga kuhudhuria mkutano huo.