Habari za Kitaifa

Raila kujiondoa kwa siasa za Kenya akichaguliwa mwenyekiti wa AUC

February 16th, 2024 2 min read

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Azimio la Umoja-One Kenya Raila Odinga sasa amefafanua kwamba ataachana na siasa za Kenya ikiwa atachaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Kwenye mahojiano na runinga ya Citizen mnamo Alhamisi usiku Bw Odinga alisema kuwa hatajishughulisha na siasa za humu nchini kwa kupindi cha miaka minne atakapohudumu katika wadhifa huo na kurejea baadaye.

“Ina maana kuwa nitalifanyia bara la Afrika kazi katika kipindi hicho ambacho nitakuwa ofisini. Haimaanishi kuwa nitajiondoa kabisa katika siasa za Kenya, lakini kwa muda huo pekee ambao nitakuwa ofisini,” akasema Bw Odinga.

Bw Odinga alieleza kuwa atakuwa amebanwa na kanuni ya utendakazi ya ofisi ya Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika inayohitaji kuwa mshikilizi wa cheo hicho ajiondoe katika siasa na kuchukua msimamo usiopendelea katika siasa za Afrika.

Ikiwa atashinda kiti hicho, Bw Odinga pia hataruhusiwa kukubali uteuzi wowote kutoka kwa serikali ya Kenya.

Mbali na masharti hayo magumu, Bw Odinga atadumisha haki yake ya kupiga kura katika uchaguzi mkuu wa 2027 lakini hatojitosa waziwazi kwenya kampeni za moja kwa moja.

Kufikia sasa, kiongozi huyo wa Azimio amepokea uungwaji mkono kutoka kwa viongozi mbalimbali nchini baada ya kutangaza wazi kuwa atashindania nafasi ya kumrithi mwenyekiti wa sasa wa AUC Moussa Faki Mahamat anayekamilisha muhula wake wa pili na wa mwisho.

Uchaguzi huo ambao utafanywa kwa kura ya siri na marais na viongozi wa nchi wanachama wa AU umeratibiwa kufanyika Julai 2024 katika makao makuu ya umoja huo jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Kwa kabisa, Bw Odinga atahitaji uungwaji mkono kutoka kwa serikali ya Kenya inayoongozwa na Rais William Ruto, hali ambayo tayari imedokezwa na Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi.

Pili, Bw Odinga atahitaji kuhakikisha amepata uungwaji mkono kutoka kwa nchi saba wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Nchi hizo zinajumuisha Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Uganda, Rwanda, Tanzania, na Sudan Kusini.

Ni baada ya hapo ambapo atapanua kampeni zake na kusaka uungwaji mkono kutoka mataifa mengi kutoka maeneo manne ya Afrika.

Maeneo hao ni Afrika Kaskazini, Afrika Magharibi, Afrika ya Kati, na Afrika Kusini.

Wakati huu ni Afrika Mashariki na Afrika Kaskazini pekee ambayo hayajawahi kutoa mwenyekiti wa AUC.

Walishikilizi wa awali walikuwa ni Amara Essy kutoka Cote d’Ivoire (Afrika Magharibi) aliyehudumu kama kaimu mwenyekiti na kuongoza mpito kutoka Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) hadi Umoja wa Afrika (AU) kati ya 2002-2003.

Pia kuna Alpha Oumar Konare wa Mali (Afrika Magharibi) aliyehudumu katika kipindi cha 2003- 2008, Jing Ping wa Gabon (Afrika Magharibi) aliyehudumu kati ya 2008-2012 huku naye Dlamini Zuma wa Afrika Kusini (Kusini mwa Afrika) akihudumu kati ya 2012-2017.

Mahamat kutoka Chad (Afrika ya Kati) ndiye ameshikilia rekodi ya kuwa mwenyekiti wa AUC kwa mihula miwili miongoni mwa watangulizi wake watano.

Amehudumu kuanzia 2017 na muhula wake wa pili unakaribia kufikia kikomo.

Akiongea na wanahabari Alhamisi baada ya kuhudhuria mkutano wa mawaziri wa mashauri ya kigeni wa mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika (AU, Bw Mudavadi alisema kwa hivi: “Japo ni maeneo ya Afrika Kaskazini na Afrika Mashariki ambayo hayajawahi kutoa mwenyekiti wa AUC, kwa kuzingatia mfumo wa alfabeti, mwaka huu ni zamu ya mtu kutoka Afrika Mashariki kuchaguliwa kwa kiti hiki.”

“Pili, kulingana na kanuni mpya zilizowekwa ni wazi kwamba Afrika Mashariki iko na nafasi bora kupata kiti hiki,” Bw Mudavadi akasema kwenye mahojiano na wanahabari jijini Addis Ababa, Jumatano.

Wiki mbili zilizopita Bw Mudavadi aliwaahidi wakazi kutoka ngome za kisiasa za Bw Odinga za Siaya na Kakamega kusubiri tangazo kubwa kutoka kwa serikali kuhusu Raila.