Habari za Kitaifa

Raila kustaafu ODM Oktoba 2024 akilenga uenyekiti AUC

Na JUSTUS OCHIENG' September 5th, 2024 2 min read

CHAMA cha Orange Democratic Movement (ODM) sasa kimeanza mipango ya Raila Odinga kustaafu rasmi kama kiongozi wake ili ajikite sawasawa katika kampeni zake za kutaka achaguliwe mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Duru katika chama hicho zimeambia Taifa Dijitali kwamba Kamati Kuu ya Usimamizi (CMC) inatarajiwa kufanya mkutano hivi karibuni kuafikia uamuzi kuhusu suala la urithi.

Bw Odinga anatarajiwa kung’atuka mapema mwezi ujao wa Oktoba, 2024, baada ya CMC kuweka taratibu na uteuzi wa kiongozi mpya.

Chama cha ODM kiliasisiwa mnamo 2005 baada ya kura ya maamuzi kuhusu rasimu ya Katiba mpya.

Upande wa “LA” uliopinga Katiba hiyo na ulioongozwa na Bw Odinga, uliwakilishwa na alama ya Chungwa (Orange kwa kimombo).

Kutokana na ushindi wa mrengo huo, Bw Odinga na wenzake waliamua kuunda chama cha kisiasa chenye jina “Orange” (Orange Democratic Movement) na wakakitumia katika uchaguzi mkuu wa 2007.

Mnamo Februari mwaka huu, 2024, Waziri huyo Mkuu wa zamani, alionyesha dalili za kujiondoka katika siasa za humu nchini alipotangaza kuwa atajitosa katika siasa za Afrika kwa kuwania wadhifa wa mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Aidha, siku chache kabla ya kuzinduliwa rasmi kama mgombeaji wa Kenya katika kinyang’anyiro hicho, Bw Odinga alisema atajiondoa katika siasa za Kenya na kuelekeza juhudi zake katika kampeni za wadhifa huo.

“Sitajishughulisha zaidi na siasa za Kenya kuanzia sasa kwani nitajikita katika kampeni za Bara Afrika. Ni awamu ya mpito kutoka siasa za Kenya hadi siasa za ngazi ya Bara Afrika,” Odinga aliambia wanahabari katika afisi ya Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi.

Sasa baada ya kuzinduliwa rasmi kama mgombeaji wa Kenya katika uchaguzi wa uenyekiti wa AUC, Taifa Dijitali imeelezwa kwamba Bw Odinga anataka kujiondoa rasmi kama Kiongozi wa Kitaifa wa ODM.

“Raila atajiuzulu kama kiongozi wa chama mwanzoni mwa Oktoba (2024). Tayari amejulisha uongozi wa chama kuhusu hatua hiyo,” mwandani mmoja wa Bw Odinga aliambia Taifa Dijitali, Jumatano, Septemba 4, 2024.

Inasemekana kuwa hatua hiyo imechochea siasa kali za urithi ndani ya chama hicho, ambavyo ni mojawapo ya vyama vyenye ufuasi mkubwa nchini.

Kuna wale wanaopendekeza kuundwe kamati ya muda kuongoza ODM hadi Februari mwaka ujao, 2024 uchaguzi wa kiti cha AUC utakapofanyika.

Lakini kwa upande mwingine, kuna wanaoshikilia kuwa mwanachama mmoja mahiri atwikwe wadhifa wa kuwa kaimu kiongozi wa ODM.