Michezo

Rais Ruto afurahishwa na ujenzi wa uwanja wa Talanta


RAIS William Ruto amesema ameridhishwa na shughuli za ukarabati zinazoendelea kwenye uwanja wa Talanta Sports City Complex, huku akitoa hakikisho kuwa uwanja huo utakamilika kabla ya mwaka ujao kumalizika ili kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).

Ruto alisema hayo Jumanne baada ya kutembelea uwanja huo unaopatikana kando ya Ngong Road, Nairobi kujionea ujenzi unaoendelea.

“Nimefika hapa leo kujionea ujenzi unaoendelea kwenye uwanja huu, na nimeridhika kuwa utamalizika wakati ufaao. Mradi huu utabainisha upya wasifu wetu kwenye kituo hiki kilichofanyiwa ukarabati wa hali ya juu kwa ajili ya kufaidi taifa nzima wa jumla,” Rais alieleza.

Rais Ruto akihutubu wakati wa uzinduzi wa ujenzi wa Uwanja wa Talanta City Sports Complex Kaunti ya Nairobi awali. PICHA| MAKTABA

“Kenya inakusudia mpango mkubwa wa kuendeleza na kutekeleza michezo ya kila aina na sekta ya ubunifu,” alisema.

“Serikali inaimarisha viwanja vya umma kote nchini ili wachezaji wapate fursa ya kujiandalia kwenye mazingara mazuri,” aliongeza.

Awali, Rais Ruto alikuwa ametembelea shule ya walemavu ya Lenana School Primary, ambapo madarasa yanaendelea kujengwa ili kudhibiti idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na shule hiyo.