Habari za KitaifaMichezo

Roho mkononi Omanyala akiwinda fainali, medali ya 100m Olimpiki

Na GEOFFREY ANENE August 4th, 2024 2 min read

MSHIKILIZI wa rekodi ya Afrika mbio za mita 100, Ferdinand Omanyala, atalenga kumaliza ukame wa miaka miwili bila taji kubwa hapo Jumapili, Agosti 4, 2024 kwenye Michezo ya Olimpiki inayopamba moto jijini Paris, Ufaransa.

Kabla ya fainali, hata hivyo, Omanyala ana kibarua kigumu katika nusu-fainali ambapo wakimbiaji wanane pekee kutoka orodha ya washiriki 26 ndio watafika fainali.

Yuko katika nusu-fainali ya tatu (mwisho) ambayo ina wakali Fred Kerley (Amerika), Kishane Thompson (Jamaica), Andre De Grasse (Canada), Abdul Hakim Sani Brown (Japan) na Zharnel Hughes (Uingereza).

Omanyala – ambaye muda wake bora ni sekunde 9.77 aliotinga mwaka 2021 – alifuzu kwa kushinda mchujo wake wa raundi ya kwanza kwa sekunde 10.08 Jumamosi.

Hata hivyo, itakuwa roho mkononi kwa sababu wapinzani wake wote katika nusu-fainali leo, wakiwemo Abdul-Rasheed Saminu (Ghana) na Benjamin Richardson (Afrika Kusini), waliandikisha muda bora kumliko katika raundi ya kwanza isipokuwa Puripol Boonson kutoka Thailand.

Kerley ni bingwa wa dunia mwaka 2022 na alipata nishani ya fedha kwenye makala ya Olimpiki yaliyopita. Thompson anajivunia kuwa mtimkaji mwenye muda bora duniani mwaka huu katika 100m (sekunde 9.77) akifuatiwa na Omanyala (9.79).

Inspekta wa polisi Omanyala – ambaye ni kama anakimbia nyumbani kutokana kuwa ni mwanariadha wa klabu ya riadha ya Miramas inayopatikana kusini mwa Ufaransa tangu Mei 26, 2023 – alishinda mataji yake makubwa ya Riadha za Afrika mnamo Juni 9, 2022 nchini Mauritius na Michezo ya Jumuiya ya Madola mnamo Agosti 3, 2022.

Tangu wakati huo, amekimbia Riadha za Dunia 2023 nchini Hungary na Riadha za Dunia za Ukumbini 2024 nchini Scotland, lakini hakupata kitu.

Omanyala, 28, hakushiriki Michezo ya Afrika 2024 jijini Accra, Ghana, mwezi Machi wala kutetea taji lake la Afrika jijini Douala, Cameroon, mwezi Juni mwaka huu.

Vile vile, Omanyala aliambulia patupu katika Riadha za Dunia za Kupokezana Vijiti 2024 mwezi Mei nchini Bahamas akishirikiana na Mark Otieno, Hesborn Ochieng na Meshack Babu.

Nusu-fainali za 100m zitaanza mida ya saa tatu na dakika tano (9:05pm) usiku leo, huku Omanyala akiratibiwa kutimka 9:23pm. Fainali pia ni leo usiku (10:50pm).