Habari

Ruto afinywa

July 5th, 2019 2 min read

Na WAANDISHI WETU

NAIBU Rais William Ruto amebanwa zaidi kisiasa baada ya kufichuka kuwa Idara ya Kupeleleza Uhalifu inataka kuwachunguza wandani wake kwenye sakata inayohusu madai ya njama ya kumuua.

Hati ya mashtaka iliyowasilishwa mahakamani na Kiongozi wa Mashtaka ya Umma, ilionyesha kuna wafuasi 256 wa ‘Tangatanga’ ambao watachunguzwa.

Wafuasi hao wa Dkt Ruto wanaojumuisha wabunge, mawaziri, maseneta, magavana miongoni mwa maafisa wengine wa ngazi za juu serikalini, wanalengwa na DCI kwa kuwa inadaiwa walikuwa kwenye kikundi cha mtandao wa kijamii wa WhatsApp kinachotambulika kama ‘Tangatanga Movement’.

Ni katika kikundi hicho ambako barua iliyodaiwa kuandikwa kwa Rais na waziri mmoja kuhusu njama hiyo ilitumwa.

Hayo yalifichuka wakati mkurugenzi wa mawasiliano ya kidijitali katika Ikulu ya Rais, Bw Dennis Itumbi alipofikishwa kortini Nairobi ikidaiwa ndiye aliyeandika na kutuma barua hiyo iliyodai kuna mawaziri waliokutana kisiri kupanga njama ya kumuua Naibu Rais.

“Kikundi hicho cha WhatsApp kiliundwa Julai 8, 2018, na kina wanachama 256. Mimi na maafisa wangu wa upelelezi tuko katika harakati za kuwaita wanachama wote wa kikundi hicho cha WhatsApp,” afisa wa DCI, Yvonne Anyango alisema kwenye hati ya kiapo.

Wakili wa Bw Itumbi, Bw Katwa Kigen alishangaa kwa nini mteja wake ndiye aliyekamatwa ilhali kuna watu wenye ushawishi mkubwa zaidi kumliko katika kikundi hicho kinacholengwa.

Hati hiyo ya kiapo ililenga kushawishi mahakama kuagiza Bw Itumbi azuiliwe kwa siku 14, lakini Hakimu Zainab Abdul akaamua atazuiliwa kwa siku tano kuwezesha uchunguzi kukamilika.

Tangu Bw Itumbi alipokamatwa Jumatano mchana, wafuasi wa ‘Tangatanga’ wameendelea kudai kuwa ni kweli maisha ya Dkt Ruto yamo hatarini na maafisa wa upelelezi wanajaribu kufanya wananchi kusahau hilo.

Mkutano

Bw Itumbi alisisitizia mahakama kwamba kulikuwa na mkutano katika Hoteli ya La Mada jijini Nairobi, ambapo njama ya kumuua Dkt Ruto ilipangwa.

Alidai ana video inayothibitisha madai hayo na akaomba ichezwe mahakamani, lakini hakimu hakujibu ombi hilo.

Bw Itumbi aliendelea kudai kuwa alipeana habari kwa DCI kuhusu mtu anayetishia maisha ya Dkt Ruto.

Sakata hiyo imeweka hatarini sifa ya Dkt Ruto kwani haijulikani kama alifahamu barua hiyo ilikuwa feki kabla ya kupiga ripoti kuihusu kwa DCI, au ni kweli alihofia maisha yake.

Ingawa Bw Itumbi ni mwajiriwa katika Ikulu, amekuwa akimhudumia zaidi Dkt Ruto tangu mabadiliko yalipofanywa kwenye idara ya mawasiliano ya Ikulu.

Alhamisi, karibu wabunge 20 wa kundi la ‘Kieleweke’ walimtaka Naibu Rais kujiuzulu kufuatia kukamatwa kwa Bw Itumbi.

 

Ripoti ya RICHARD MUNGUTI, VALENTINE OBARA, CHARLES WASONGA na MAUREEN KAKAH