Habari za Kitaifa

Safaricom yalalamika bilionea Musk anavuruga biashara Kenya

Na DOMINIC OMONDI August 24th, 2024 1 min read

KAMPUNI ya huduma za mawasiliano, Safaricom, imeanzisha vita na Starlink ya bilionea wa Amerika Elon Musk.

Hii ni baada ya kuitaka serikali kufikiria upya uamuzi wake wa kutoa leseni kwa kampuni za kutoa huduma za mtandao kupitia satelaiti.

Safaricom iliitaka Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya (CA) kutathmini upya uamuzi wake wa kutoa leseni kwa kampuni za huduma za mtandao kupitia Satelaiti, ikionya kuwa mpango huo unaweza kuruhusu uunganishaji usio halali na kuingiliwa kwa mitandao ya simu.

Idadi ya Wakenya wanaotumia mtandao wa satelaiti imeongezeka tangu Starlink, kampuni tanzu ya kampuni ya Musk ya SpaceX, ilipoingia Kenya Julai 2023.

Lakini Safaricom inataka kampuni za huduma za satelaiti kushirikiana na kampuni za humu nchini za mtandao badala ya kampuni kama Starlink kujitegemea, ikisema kwamba kuingia kwao moja kwa moja nchini kunahatarisha ubora wa mtandao wa simu za rununu.

‘Safaricom inaomba Mamlaka ya Mawasiliano ya Kenya kutathmini kwa makini hatari za kutoa leseni huru kwa watoa huduma za satelaiti na madhara ambayo inaweza kusababisha Kenya,’ ilisema Safaricom katika barua kwa Afisa Mkuu Mtendaji wa CA, David Mugonyi.