Habari za Kaunti

Sakaja aahidi kuboresha viwanja vya michezo Nairobi kukuza vipaji

Na WINNIE ONYANDO September 5th, 2024 1 min read

GAVANA wa Nairobi, Johnson Sakaja ameahidi kujenga na kukarabati viwanja zaidi vya michezo kama njia ya kuwezesha vijana kukuza talanta zao na kuboresha maisha yao ya baadaye.

Gavana huyo alisema kuwa serikali yake inajitahidi sana kuboresha baadhi ya viwanja vya michezo katika kaunti yake.

Bw Sakaja alizindua uwanja wa michezo wa Dandora Machi 8, 2024 baada ya ujenzi wake kuchukua miaka sita.

“Serikali yangu itakarabati viwanja zaidi ili vijana wetu waweze kukuza vipaji vyao,” Bw Sakaja alisema alipokuwa akizindua uwanja huo.

Uwanja huo ulio na uwezo wa kusitiri watu 4,000 umekarabatiwa ipasavyo, na vilevile kuundwa na vifaa ya kisasa.

Unawawezesha vijana kuwa na jukwaa la kuimarisha, kukuza na kuboresha vipaji vyao.

Bw Sakaja pia alizindua Uwanja wa Michezo wa Uhuru Complex, ambao unaweza kutumika kwa michezo ya netiboli, voliboli na kandanda.

Pia, una ukumbi wa michezo ya ndani kama chess, na tenisi, kati ya michezo mingine.

Unatoa fursa kwa vijana kuonyesha uwezo wao katika taaluma mbalimbali za michezo.

Viwanja vingine vilivyotengwa kwa ajili ya ukarabati na ujenzi, ni pamoja na Uwanja wa Kihumbui, ambao ujenzi wake ulizinduliwa na Gavana Sakaja mwaka huu, 2024, ujenzi wa Uwanja wa Woodley Ziwani, Githurai, Mukuru, na zingine.

Gavana Sakaja anaamini kuwa hatua kama hizo zitawafaidi vijana ambao wana vipaji mbalimbali.