Habari za Kitaifa

Seneta ataka waathiriwa U-18 wa ukatili wajaziwe fomu ya P3 bila ada

January 12th, 2024 2 min read

NA MWANGI MUIRURI

SENETA wa Murang’a Bw Joe Nyutu amependekeza fomu ya P3 ambayo hupeanwa na vituo vya polisi iwe ikijazwa hospitalini bila malipo yoyote kwa waathiriwa wote wa ukatili walio chini ya miaka 18.

Alisema kwamba wengi wa waathiriwa wa ukatili kama wa kubakwa au kulawitiwa pamoja na kupigwa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18 huwa ni wa kutoka familia maskini.

Fomu hiyo hutumika katika kuelezea kiwango cha ukatili uliotekelezewa mwaathiriwa na hujazwa na afisa wa afya aliyehitimu na ambaye anahudumu katika hospitali ya umma ya Level 4 kuenda juu.

Maelezo katika fomu hiyo ya P3 hutumika kama ushahidi kortini na afisa aliyeijaza huorodheshwa kama shahidi wa kitaalamu mahakamani.

“Hospitali nyingi hudai kuanzia Sh1,500 kuenda juu zikisema ni ada ya kugharimia usafiri wa afisa aliyeijaza hadi mahakamani kutoa ushahidi. Afisa huyo akirejea kazini huwa anajaza fomu ya kurejeshewa gharama zake na pia kulipwa marupurupu,” akasema seneta Nyutu.

Bw Nyutu alikuwa akiongea katika eneobunge la Kigumo mnamo Januari 9, 2024, kulikoandaliwa hafla ya shukrani kwa Mungu kwa kuwezesha shule ya sekondari ya Karega kufanikiwa na matokeo bora ya KCSE ambapo wanafunzi 100 walipata gredi ya kujiunga na vyuo vikuu nchini.

Aliongeza kwamba maafisa hao pia hurejeshewa gharama za usafiri na mahakama “kwa hivyo ada hiyo ambayo wao hudai waathiriwa wa ukatili huwa ni haramu na isiyofaa kutozwa”.

Bw Nyutu alisema kwamba “watoto wa maskini hujipata wakikosa haki kwa kuwa hawakupata pesa za kujaza P3 na ambayo hakuna kesi inaweza ikazinduliwa bila ukadiriaji huo muhimu wa majeraha na afisa wa afya”.

Alisema kwamba “ukichunguza visa vya watoto zaidi ya 3,000 ambao walikuwa wamesajiliwa kufanya mtihani wa kidato cha nne mwishoni mwa 2023 lakini wakakosa kufika katika vituo vya mtihani huenda walijipata katika ukatili wa kushambuliwa na kudhulumiwa hadi wakalemewa kuendelea mbele na masomo”.

Seneta Nyutu alisema “bila shaka kunao walidhulumiwa na wabakaji pamoja na walawiti, wengine pia wakiathirika kwa mashambulio ya kila aina”.

Bw Nyutu alisema kwamba “kesi za aina hiyo zikihusisha watoto zinafaa kugharamiwa na serikali kupitia ushirikishi wa kamanda wa polisi (OCS) katika kituo ambacho kesi hiyo iliripotriwa kwa ushirikiano pia wa Mkuu wa tarafa (ACC) wa eneo hilo”.

Alisema hali hiyo inafaa kuwa sera ili kuhakikishia waathiriwa wote wa chini ya miaka 18 haki kwa mujibu wa sheria ya kulinda watoto nchini.

“Kama mwenyekiti wa kamati ya Seneti kuhusu elimu, nitasukuma mjadala huu hadi ndani ya sera za wizara ili wakati unadhulumu mtoto wa masikini na unatumia unyonge wa familia yao wa kugharamia kesi, uwe ukielewa utabishana na serikali moja kwa moja,” akasema Bw Nyutu.

Alisema kwamba kuna visa vingi ambavyo havikuwahi kupata haki kwa kuwa wazazi walikosa pesa za kugharamia fomu hiyo na pia matibabu dhidi ya majeraha.

[email protected]