Habari za Kitaifa

Serikali yaahidi kutoa vitambulisho vya kitaifa ndani ya siku 10


UTAPATA kitambulisho chako cha kitaifa siku 10 baada kuwasilisha maombi ikiwa ahadi mpya iliyotolewa na serikali itatimizwa.

Katibu wa Wizara anayesimamia Idara ya Uhamiaji na Huduma za Raia Julius Bitok Jumatatu, Septemba 16, 2024, alisema hilo litawezekana kuanzia Oktoba 1, 2024 baada ya idara yake kuweka mitambo bora ya kunasa picha za watu na maelezo katika vituo vyote vya Huduma Centre na Afisi za Kitengo cha Usajili wa Watu (NRB).

Vile vile, NRB imeimarisha uwezo wake wa kuchapisha vitambulisho kufuatia kununuliwa kwa mashine mbili mpya za uchapishaji.

Hali hii inafupisha muda wa kupatikana kwa vitambulisho vya kitaifa.

“Kuanzia Oktoba 1, mwaka huu wale waliowasilisha maombi ya vitambulisho vipya hawatasubiri kwa zaidi ya siku 10 kabla ya kuvipata. Hii ni kinyume na siku 21 za awali. Tunataka kuhakikisha kuwa Wakenya wanapata stakabadhi hizi haraka iwezekanavyo,” Dkt Bitok akasema wakati wa hafla ya maadhimisho ya Siku ya Kitambulisho Duniani (World ID Day).

Maadhimisho ya mwaka huu yalifanyika katika kituo cha kibiashara cha Katoloni, Kaunti ya Machakos.

Siku hiyo, Septemba 16, imetengwa kwa ajili ya kutoa uhamasisho kuhusu umuhimu wa vitambulisho vya kitaifa na stakabadhi zingine muhimu kama vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya mienendo bora miongoni mwa vingine.

Katika shughuli ya mwaka huu, watu ambao hawana stakabadhi hizo walijaza fomu za maombi ya vitambulisho vya kitaifa, vyeti vya kuzaliwa, vyeti vya mienendo bora, paspoti miongoni mwa stakabadhi nyinginezo.