Michezo

Shujaa kikaangoni droo ya Hong Kong Sevens ikitangazwa

March 11th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya raga ya wachezaji saba kila upande ya Kenya almaarufu kama Shujaa, imekutanishwa na miamba Fiji, New Zealand na Australia katika Kundi C kwenye duru ya Hong Kong Sevens itakayofanyika Aprili 5-7, 2019.

Vijana wa Paul Murunga wataelekea Hong Kong wakiwa katika nafasi ya 14, nafasi moja kutoka nafasi ya 15 ambayo ni ya kutemwa na kwa sasa inashikiliwa na Japan. T

Wafiji walinyakua ubingwa wa Hong Kong Sevens mwaka 2018 kwa kuchabanga Kenya 24-12 katika fainali. Wanavisiwa hawa wanashikilia nafasi ya tatu msimu huu na wametwaa mataji ya Cape Town nchini Afrika Kusini na Hamilton nchini New Zealand. Mabingwa wa duru za Dubai na Sydney, New Zealand wako katika nafasi ya pili baada ya kuzoa alama 106. Wako alama tano mbele ya Fiji. Australia, ambayo ilifika nusu-fainali mjini Dubai, iko katika nafasi ya sita kwa alama 65.

Wakenya wamekuwa wakiishi katika maeneo hatari msimu wote, na droo ya Hong Kong bila shaka inawaweka mahali pabaya zaidi inapopambana kukwepa kuangukiwa na shoka. Shujaa imeshiriki duru zote tangu msimu 2002-2003. Hata hivyo, mambo huenda yakabadilika baada ya msimu huu kwa sababu dalili inaendelea kuning’inia pabaya.

Iliandikisha historia yake nzuri kabisa katika mashindano haya ya kifahari msimu uliopita pale ilipoingia alama 100 baada ya kuzoa alama 104.

Kenya, ambayo iko alama nne pekee juu ya nambari 15 Japan baada ya duru sita za kwanza, inatarajiwa nchini Machi 12 usiku kutoka ziara ya Amerika Kaskazini ilikoambulia alama tano mjini Las Vegas nchini Marekani mnamo Machi 3 na pointi moja kutoka mjini Vancouver nchini Canada mnamo Machi 10.

Mabingwa wa Vancouver Sevens Afrika Kusini wameorodheshwa wa kwanza mjini Hong Kong na kutiwa katika Kund A pamoja na Samoa, Scotland na Japan. Ufaransa, ambo walipoteza 21-12 dhidi ya Afrika Kusini katika fainali ya Vancouver, wako katika Kundi B pamoja na Argentina, Canada na waalikwa Ureno, ambao waliwahi kushiriki Raga ya Dunia kabla ya kupoteza nafasi yao mwaka 2016.

Viongozi wa msimu huu Marekani wako katika Kundi D pamoja na Uingereza, Wales na Uhispania.