Habari

SI AJALI, NI MAUAJI

October 11th, 2018 2 min read

Na ANITA CHEPKOECH

UKIUKAJI mkubwa wa sheria za trafiki na ujeuri wa wahudumu wa basi ndio uliosababisha vifo vya watu 55 katika eneo la Fort Ternan kwenye barabara ya Londiani – Kericho Jumatano alfajiri.

Kulingana na simulizi za walionusurika, wakazi wa eneo la Fort Ternan na polisi, abiria hao wangekuwa hai iwapo sheria za barabarani hazingekiukwa kiholela.

Kulingana na walionusurika, basi hilo lilikuwa likiendeshwa kwa kasi sana, jambo ambalo lilikuwa kiini kikuu cha ajali hiyo. Hii ni kutokana na kuwa gari likiwa mwendo wa kasi inakuwa vigumu kwa dereva kulithibiti iwapo hatari yoyote itatokea.

Abiria hao walisema basi hilo lililokuwa likielekea Magharibi kutoka Nairobi, lilianza kuendeshwa kasi kuanzia Naivasha na walipolalamika walirushiwa matusi na makanga watundu.

Kulingana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usalama Barabarani (NTSA), Bw Francis Meja, basi hilo halikuwa na leseni ya kuhudumu usiku.

Hili linazua maswali jinsi lilivyoweza kubeba abiria katika kituo cha mabasi cha Machakos jijini Nairobi huku wasimamizi wa kampuni ya Western Cross Express wakifahamu walikuwa wakivunja sheria. Ajali nyingi hasa zinazohusisha mabasi hutokea usiku kutokana na matatizo ya uendeshaji kukiwa na giza.

Habari pia zilidokeza kuwa basi hilo lilikuwa limebeba abiria kupita kiasi, jambo ambalo huwa hatari kutokana na gari kukosa udhabiti. Ilidokezwa kuwa lilipofika Westlands viungani mwa Nairobi likielekea Magharibi, lilirudi Machakos na kuchukua abiria zaidi kutoka kwa basi lingine.

Haya yanaibua maswali kuhusu maafisa wa polisi wa trafiki ambao huwa wengi kwenye barabara ya Nairobi-Naivasha-Nakuru. Maafisa hao wana wajibu wa kuhakikisha magari ya uchukuzi wa umma yanazingatia sheria, na hivyo haieleweki ni kwa nini hawakutambua basi hilo halikuwa na leseni ya kuhudumu usiku na pia lilikuwa limebeba abiria kupita kiasi.

NTSA pamoja na washikadau wengine katika sekta ya uchukuzi wa umma pia ni wa kulaumiwa kwa kuchelewa kupata suluhisho kwa suala la kanuni mpya za ujenzi wa mabasi zilizoanza Mei 2017.

Licha ya kanuni hizo kuanza, mabasi ya kabla ya hapo yangali na udhaifu uliokuwepo.

Wizara ya Barabara pia ilichangia vifo vya ajali ya jana kutokana na ujenzi mbaya wa barabara ya Londiani-Muhoroni. Wakazi wa Fort Ternan walisema wameshuhudia ajali 20 mwaka huu katika eneo hilo kutokana na barabara hiyo kuwa mbaya.

Ajali zilizosababisha vifo vya watu wengi

DESEMBA 11, 2016
Abiria 40 walichomeka hadi kufa baada ya lori lilokuwa limebeba kemikali kugonga magari kadhaa na kulipuka eneo la Karai viungani mwa mji wa Naivasha.

DESEMBA 12, 2017
Watu 19 walipoteza maisha katika barabaraya Kitale-Webuye wakati matatu ilipotumbukia katika Mto Kamukuywa baada ya kugonga lori.

DESEMBA 17, 2017
Watu 17 walikufa katika barabara ya Thika-Garissa wakati matatu ya Kinatwa Sacco ilipogongana na lori eneo la Kilimambogo. Matatu hiyo ilikuwa imetoka Nairobi kuelekea Kitui.

Abiria 10 walikufa baada ya lori kugongana na matatu waliyokuwa wakisafiria katika makutano ya Eldama kuelekea mjini Eldoret.

DESEMBA 31, 2017
Abiria 30 walipoteza maisha na wengine 16 wakajeruhiwa eneo la Migaa katika barabara kuu ya Nakuru-Eldoret wakati basi la Matunda Sacco lilipogongana na lori likielekea Busia kutoka Nairobi.

APRILI 11, 2018
Abiria 19 walifariki basi la Daima Connection Sacco lilipotumbukia katika Mto Siyiapei kwenye barabara ya Narok-Maai Mahiu likielekea Nairobi kutoka Kendu Bay.

AGOSTI 5, 2018
Wanafunzi 10 waliangamia na wengine 27 kujeruhiwa vibaya baada ya basi yao ya shule kugongwa na lori karibu na mji wa Mwingi, Kaunti ya Kitui. Wanafunzi hao wa shule ya msingi ya St Gabriel walikuwa wametoka ziara Mombasa wakati walipopata ajali hiyo wakikaribia nyumbani.