BBI: Wanasiasa wang'ang'ania vinono
CECIL ODONGO Na BENSON MATHEKA
Wanasiasa wanaendelea kung’ang’ana ili kuhakikisha kwamba maslahi yao yanazingatiwa kabla ya ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) kupitishwa kwenye kura ya maamuzi.
Magavana, wabunge na wawakilishi wa wadi wanaendelea kutoa mapendekezo kuhusu masuala ambayo wanahisi yatawanufaisha katiba ikifanyiwa mageuzi kupitia mchakato huo.
Kwa upande wao, madiwani kupitia Muungano wao wa Wawakilishi Wadi (CAF) wanataka watengewe hazina inayojumuisha asilimia 30 ya mgao wa kaunti kinyume na pendekezo kwenye BBI inayotaka wapewe asilimia tano pekee.
“Tunataka fedha ambazo zimetengewa wadi ziongezwe kutoka asilimia tano hadi 30. Ripoti hiyo ihakikishe kwamba bajeti ya wadi haziingiliwi na usimamizi wa kaunti,” akasema Bw Ndegwa.
Wawakilishi wadi wamekuwa wakisisitiza kwamba katiba ya sasa inawapa magavana mamlaka makubwa ya kudhibiti fedha za kaunti na mara nyingi hutumia hali hiyo kuwahonga madiwani ili waunge mkono ajenda zao.
Madiwani pia wanataka wawe wakiteuliwa kuwa mawaziri wa kaunti jinsi wabunge watakuwa wakiteuliwa kuwa mawaziri katika serikali kuu.
Nao wabunge, mbali na kuahidiwa kuwa na usemi katika hazina ya maeneobunge, watakuwa na nafasi ya kuteuliwa mawaziri. Pia watakuwa na nguvu za kuamua mgao wa pesa kwa kaunti jukumu ambalo lilipokonywa seneti. Maseneta pia wanataka wawe wakiteuliwa katika baraza la mawaziri wakisema wao ni sehemu ya bunge.
Ingawa wamepokonywa jukumu muhimu la kuamua mgao wa serikali za kaunti, maseneta wanataka wapatiwe mamlaka zaidi kuliko wabunge.
Wabunge ambao wamekuwa wakisimamia fedha za Hazina ya Maeneobunge (CDF) nao wamekuwa wakitaka pia wapokezwe mgao wa kaunti ili wasimamie miradi kwenye maeneo yao.
Magavana wanataka wawe wakiwachagua manaibu magavana baada ya uchaguzi mkuu kinyume na sasa ambapo huwa ni wagombea wenza wao. Iwapo pendekezo hilo litakumbatiwa, basi magavana watakuwa na uhuru wa kuwatimua manaibu wao jinsi wanavyofanya mawaziri wanasosimamia idara mbalimbali katika serikali za kaunti zao chini ya katiba ya sasa.
Aidha wamepinga pendekezo kwenye BBI la kuwashurutisha wateue manaibu gavana wa jinsia tofauti, wakisema hilo halitawezesha wanawake wengi kushikilia nyadhifa hizo.
La muhimu kabisa hata kwa viongozi hao wa kaunti ni kwamba, BBI imruhusu Mdhibiti wa Bajeti atoe fedha za kaunti bila mchakato unaohusu Mswada wa Mgao wa Fedha kupitishwa kwanza na Seneti na Bunge la Kitaifa.
Hii inatokana na kuchelewa kwa fedha za kaunti mara kwa mara huku mabunge hayo mawili yakijikita kwenye ubabe kuhusu bajeti nzima kwa kaunti zote 47.
Mwenyekiti wa Baraza la Magavana (COG) Wycliffe Oparanya hata hivyo, anasisitiza kwamba, nia yao ya kupigania matakwa hayo ni kufanya ugatuzi uwe thabiti kinyume na sasa ambapo umezingirwa na vizingiti kadhaa.