• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Chunga sana Raila, Ruto ashauriwa

Chunga sana Raila, Ruto ashauriwa

NA JAMES MURIMI

VIONGOZI wa Mlima Kenya wamemtaka Rais William Ruto ajihadhari hata anaposhirikiana na Bw Raila Odinga kisiasa, wakisema huenda kinara huyo wa upinzani anaweza akatumia uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC) kusambaratisha utawala wa Kenya Kwanza.

Wakati huo huo, viongozi hao walisema “watasimama nyuma ya Naibu Rais Rigathi Gachagua” hata kama ushirikiano kati ya Rais na Raila utamtenga.

Bw Odinga ametangaza azma yake ya kuwania kiti cha AUC hapo Januari 2025 naye Rais Ruto ametangaza hadharani kuwa serikali yake itamuunga mkono.

Soma Pia: Jinsi azma ya Raila AUC inavyozima ndoto za wanasiasa Mlimani – Uchambuzi

Hata hivyo, Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga alisema waziri huyo mkuu wa zamani ni mwanasiasa mjanja ambaye anastahili kufuatiliwa kwa makini akifanya kampeni ya kupata kazi ya AUC.

Gavana huyo alisema anaunga mkono nia ya kinara huyo wa upinzani ila anahofia atacheza “karata yake ya kisiasa kuvuruga uthabiti wa serikali ya Kenya Kwanza”.

“Tunamwambia Rais wetu awe chonjo huku akimsaidia Raila kufanya kampeni ya kusaka kazi ya AU. Raila ni mkubwa wetu na tunampenda ila kila wakati akikaribia kupata mamlaka, yeye huvuruga serikali iliyoko mamlakani,” akasema Bw Kahiga.

Gavana huyo alikuwa akiongea wakati wa mazishi ya Samuel Mwangi, babake Diwani wa Ol Moran George Karuiri. Mazishi hayo yalifanyika katika kijiji cha Gitero, eneobunge la Tetu, Kaunti ya Nyeri.

“Tunamuunga mkono apate kazi ya AU lakini asitumie wadhifa huo kusambaratisha umoja wa serikali au kuivuruga kwa kuingia kwa mlango wa nyuma. Sisi tulimchagua Rais na naibu wake Rigathi na wanastahili kusalia na umoja wao,” akaongeza.

Wiki jana, Rais na Bw Odinga walikutana na Rais wa Uganda Yoweri Museveni nyumbani kwake Kisozi, Uganda.

Wakati wa mkutano huo, azma ya Bw Odinga ya AUC ilijadiliwa pamoja na uhusiano wa kibiashara kati ya Kenya na Uganda.

Mkutano huo uliwachemsha nyongo baadhi ya wanasiasa wa Mlima Kenya ambao waliuona kama mbinu ya kumtenga Bw Gachagua serikalini.

Naibu wa Rais mwenyewe hajazungumza hadharani kuhusu uwaniaji wa Bw Raila, hali inayoibua madai kuwa hajachangamkia nia yake.

Kauli ya Bw Kahiga iliungwa mkono na Mbunge wa Laikipia Magharibi Wachira Karani ambaye alihutubu pia katika mazishi hayo.

“Juzi tuliona wilbaro ikibeba machungwa Uganda. Kama watu wa eneo hilo lazima tuungane nyuma ya Gachagua. Lazima tumakinike kwa sababu tukitofautiana, kuna dalili kubwa tutapoteza,” akasema Bw Karani.

Mbunge huyo alisema bayana kuwa ni jamii ya Agikuyu ndiyo itahasirika katika maridhiano kati ya Rais na Bw Raila.

Mwakilishi wa Kike wa Laikipia Jane Kagiri alisema Mlima Kenya unatambua Bw Gachagua kama kiongozi wao na watapinga juhudi zozote za kumtenga serikalini.

“Rigathi ni mtoto wetu kwa hivyo lazima tuungane nyuma yake,” akasema Bi Kagiri.

Hata hivyo, Kiongozi wa TSP Mwangi Kiunjuri alitofautiana na wanasiasa hao akisema hawana mamlaka ya kumuamulia Rais Ruto viongozi ambao anaunda nao urafiki.

“Tusianzishe vita hewa na najua hamtakubaliana na mimi ila nina haki ya kusema maoni yangu. Nimekuwa kwa siasa kwa miaka mingi na kama kuna hila kati ya kutenga eneo hili, ningekuwa nishajua,” akasema mbunge huyo wa Laikipia Mashariki.

Gavana wa Laikipia Joshua Irungu na Seneta John Kinyua pia walieleza hofu yao kuwa uhusiano wa Bw Odinga na Ruto utachangia Mlima Kenya kutengwa serikalini.

  • Tags

You can share this post!

Mwanamke aliyeombewa na mhubiri ‘tata’ ajipa...

Kipruto azima Kipchoge na kuvunja rekodi mbio za Tokyo...

T L