GHASIA ZA MURANG'A: Mutyambai aonya wanasiasa
Na CHARLES WASONGA
INSPEKTA Jenerali wa Polisi Hillary Mutyambai Jumapili alitoa onyo kali kwa wanasiasa akiwataka kukosa kuchochea fujo na kuvuruga amani nchini.
Hii ni baada ya ghasia kushuhudiwa majira ya asubuhi Naibu Rais William Ruto alipozuru eneo la Kenol, Kaunti ya Murang’a kwa ibada na halfa ya kuchanga fedha.
Dkt Ruto alikuwa ametembelea kanisa la African Independent Pentecostal Church of Africa (AIPCA), kwa mwaliko wa Mbunge wa Kandara, Alice Wahome.
Bw Mutyambai alitoa onyo hilo huku wanasiasa wa Murang’a wakielekezewa kidolew cha lawama kwa kuchochea fujo hizo zilizosababisha vifa vya watu wawili.
“Tunawaka wanasiasa kukoma kutoa matamshi ya uchochezi. Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayepatikana na hatia ya kupanga au kushiriki vitendo vya kuvunja sheria, akasema.
Mutyambai pia ameamuru kikosi maalum cha maafisa wake wachunguze fujo za kisiasa zilizotokea Jumapili katika eneo la Kenol, Kaunti ya Murang’a ambapo watu wawili walifariki.
Alieleza kuwa ameagiza mkurugenzi wa Kitengo cha Masuala ya Ndani (IAU) na maafisa wawili wa upelelezi wa jinai (DCI) kuchunguza ghasia hizo kwa lengo la kuwakamata wahusika.
Wakati huo huo, Dkt Ruto ameomba msamaha kwa waumini wa kanisa hilo la AIPCA ambako gesi ya kutoa machozi ilirushwa wakati wa fujo hizo.
“Wale waliotoa amri waumini warushiwe vitoa machozi ni watu wanaofanya kazi chini yetu. Kwa hivyo, ningependa kuomba msamaha kwa AIPCA na makanisa yote nchini kutokana na vitendo vya aibu kama hivi,” akasema.
Wabunge Ndindi Nyoro (Kiharu) na Alice Wahome waliwashutumu wanasiasa wa Murang’a wakiongozwa na Mbunge Mwakilishi wa Sabina Chege kwa kudhamini fujo hizo.