JAMVI: Ruto anavyotembea njia ya masulubisho kisiasa
Na MWANGI MUIRURI
SI siri kuwa wandani wa Rais Uhuru Kenyatta hawana nia ya kumuunga mkono Naibu wa Rais, Dkt William Ruto kurithi urais katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Ni suala ambalo shaka ni finyu kuwa Dkt Ruto atatwaa tiketi ya chama cha Jubilee katika mchujo wa mwaniaji wa urais na hatimaye kujipa uungwaji mkono wa vyombo vya mamlaka vya serikali katika kampeni za urais.
Hata hivyo, uwepo wa nia ya kumsaliti na kumtema Ruto umedhihirika wazi, lakini mtihani sasa utakuwa jinsi ya kumweka katika mkondo wa kupoteza imani ya Wakenya ambao ndio wamiliki wa kura za kumpa urais au wamnyime.
“Tunajua kuwa kuna kazi ya kufanywa ili DP Ruto aishie kutemwa na wapiga-kura waelewe kisawasawa kuwa hatakosa urais kwa msingi mwingine wowote bali ni kwa manufaa ya utawala bora kwa Wakenya,” asema naibu mwenyekiti wa Jubilee, David Murathe.
Murathe anasisitiza kuwa “kwa sasa hoja si kama Dkt Ruto atakuwa mrithi wa urais 2022 bali ni vipi atakavyopingwa asikaribie ikulu kwa kuwa si chaguo la Jubilee ama Rais Uhuru wala wafuasi wa Jubilee na Rais, hasa katika ukanda wa Mlima Kenya”.
Anasema kuwa Ruto amekuwa akijijenga sana katika ngome ya Rais Uhuru ya Mlima Kenya “na hivi karibuni tunaingia huko kusambaratisha umaarufu ambao amekuwa nao eneo hilo na tutaunganisha wapiga-kura wa Mlima Kenya kumsusia DP Ruto katika ushindani wa 2022”.
Wadadisi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa mitego tele imekuwa ikiwekwa katika barabara ya kisiasa ya Dkt Ruto ili anaswe na ajikwae lakini hadi sasa haijaonekana kufaulu.
Mhadhiri wa Somo la Sayansi ya Kisiasa Gasper Odhiambo anasema kuwa “kufaulu au kuanguka kwa Ruto kisiasa kunategemea pakubwa jinsi atakavyokwepa njama za kumnasa anazoandaliwa katika barabara yake ya kisiasa.”
Anasema kuwa Ruto anafaa kuwa tayari kwa mitego hata ya kuandaliwa kura ya kukosa imani naye katika njama ya kumng’atua, kuzinduliwa kwa uchunguzi dhidi yake kuhusu unyakuzi wa ardhi na biashara za wenyewe na hata kuandaliwa kesi kuhusu madai ya ufisadi na mauaji.
Bw Odhiambo anasema kuwa kesi na madai kwa sasa dhidi ya Dkt Ruto si lazima ziwe na ukweli bali “ni katika njama za kipropaganda ambazo hukubalika kama mbinu mwafaka katika mieleka ya kisiasa.”
Aliyekuwa mbunge wa Maragua Elias Mbau anasema kuwa “ni kweli tumekuwa tukimwekea Dkt Ruto mitego kadhaa ya kisiasa lakini jinsi amekuwa akiiruka inaashiria kuwa hapa kuna kazi kubwa ambayo lazima ifanywe ili mpango huu ufaulu”.
Anasema kuwa hili halifanywi kwa nia mbaya dhidi ya Ruto kama binadamu bali “ni dhidi ya upungufu wake wa kuaminika na uongozi wa kitaifa”.
Anasema kuwa mitego hiyo imekuwa kwa msingi wa kuangazia visa tele vya ufisadi ambao huhusishwa na Dkt Ruto, kumwangazia kama asiye na nia ya amani nchini kufuatia pingamizi zake kwa handisheki ya Machi 2018 kati ya Rais na aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, kuwinda wandani wake katika nyadhifa mbalimbali serikalini na kuwang’atua na pia kumwangazia kama mlafi wa mamlaka ya kisiasa kwa kuandaa kampeni za mapema.
“Ndiyo ninakubali kuwa jinsi mikakati hii imetekelezwa imekuwa na matokeo duni hadi sasa na hakuna ushahidi kuwa Dkt Ruto amepondeka kisiasa jinsi tunavyotaka. Ningetaka ieleweke kuwa hatumpingi kwa msingi mwingine wowote bali ni kwa ule wa kukinga taifa hili kuongozwa na rais ambaye ataishia kupora nchi na kuigeuza kuwa ya kutenga Wakenya wengi kikabila,” asema Mbau.