• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 4:42 PM
JAMVI: Sura za kikosi cha Ruto katika BBI

JAMVI: Sura za kikosi cha Ruto katika BBI

Na WANDERI KAMAU

KUFUATIA uzinduzi wa ripoti ya Jopokazi la Maridhiano (BBI) na Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, sasa ni dhahiri kivumbi cha ripoti hiyo kimeanza rasmi kati ya upande unaoiunga mkono na wale wanaoipinga.

Rais Kenyatta na Bw Odinga wanawategemea magavana, maseneta, wabunge na wanasiasa wengine maarufu kuendesha kampeni za kuipigia debe katika maeneo mbalimbali nchini.

Sawa na mkakati kama huo, ripoti zinaeleza Naibu Rais William Ruto anawategemea waandani wake katika sehemu mbalimbali kuendesha kampeni za kuipinga ripoti hiyo, ikiwa matakwa yao hayatazingatiwa.

Je, sura za viongozi watakaoendesha kampeni hizo ni zipi?

Kulingana na mpangilio wa kuipigia debe ripoti katika kambi ya Rais Kenyatta na Bw Odinga, duru zinasema wawili hao wanawategemea wataalamu na wanasiasa kuvumisha juhudi hizo.

Tayari, wamebuni kundi maalum la wataalamu ambao watapiga jeki juhudi za wanasiasa kuipigia debe ripoti hiyo katika maeneo wanakotoka.

Kundi hilo linawashirikisha wakili Tom Macharia, Prof Ben Shihanya, wakili Faith Waigwa, Bw Stephen Mwachofi, Dkt Ken Nyaundi, Prof Lawrence Gumbe na Prof Isaiah Kindiki.

“Wataalamu hao watahusika katika kubuni mikakati mipya kuhakikisha kampeni ya kuipigia debe ripoti imefaulu,” akaeleza wakili Paul Mwangi, ambaye alihudumu kama Katibu wa jopo lililoongozwa na Seneta Yusuf Haji wa Garissa.

Kimaeneo, wawili hao pia watawategemea washirika wao kuhakikisha kampeni za ripoti zimefaulu.

Katika eneo la Magharibi, bendera ya wawili hao itaongozwa na kiongozi wa Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi, kiongozi wa Ford-Kenya, Bw Moses Wetang’ula na Gavana Wycliffe Oparanya wa Kakamega.

Katika eneo la Mashariki, juhudi hizo zitaendeshwa na kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka na Gavana Charity Ngilu wa Kitui.

Katika ukanda wa Pwani, watakaovumisha kampeni ya BBI ni magavana Hassan Joho (Mombasa), Amason Kingi (Kilifi) na Seneta Maalum Agnes Zani.

Bonde la Ufa, wale wamepewa jukumu hilo ni Seneta Gideon Moi (Baringo) ambaye pia ndiye kiongozi wa Kanu, kiongozi wa Chama Cha Mashinani (CCM) Isaac Rutto na Gavana Alex Tolgos (Elgeyo Marakwet).

Mlima Kenya, watakaoongoza kampeni ni magavana Anne Waiguru (Kirinyaga), Kiraitu Murungi (Meru), Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Amos Kimunya, Kiongozi wa Wengi kwenye Seneti Irungu Kang’ata na mwanasiasa Peter Kenneth.

Katika eneo la Nyanza, juhudi zitaongozwa na Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, Seneta James Orengo (Siaya) na Gavana James Ongwae (Kisii).

Dkt Ruto pia amewajumuisha wataalamu kadhaa, ambao juhudi zao zitaoanishwa na mikakati ya wanasiasa.

Baadhi ya wataalamu ambao wanatarajiwa kupiga jeki harakati za Dkt Ruto ni mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Barrack Muluka, Mkuu wa Kitengo cha Masuala ya Sheria katika afisi yake, Dkt Korir Sing’oei, Bw Eliud Owallo kati ya wengine.

Duru zinasema Dkt Ruto bado anaendelea na mikakati kuwasaka wataalamu zaidi, ambapo kando na kuweka juhudu kuhusu kampeni za kuipinga ripoti ya BBI, watamsaidia pakubwa kuweka juhudi kuimarisha kampeni kuwania urais 2022.

Katika eneo la Magharibi, Dkt Ruto anawategemea wanasiasa Benjamin Washiali (mbunge, Mumias Mashariki), aliyekuwa Seneta wa Kakamega Boni Khalwale, aliyekuwa Waziri wa Michezo Rashid Echesa kati ya wanasiasa wengine.

Katika ukanda wa Mashariki, atawategemea aliyekuwa Seneta wa Machakos Johnstone Muthama, wabunge Victor Munyaka (Machakos Mjini), Nimrod Mbai (Kitui Mashariki), aliyekuwa Naibu Gavana wa Machakos Bernard Kiala miongoni mwa wengine.

Pwani, Dkt Ruto anawategemea wabunge Aisha Jumwa (Malindi), Mohamed Ali (Nyali), aliyekuwa Seneta wa Mombasa Hassan Omar, aliyekuwa Gavana wa Taita Taveta John Mruttu miongoni mwa wengine.

Ingawa anajivunia udhibiti wa kisiasa wa eneo la Bonde la Ufa, duru zinaeleza Dkt Ruto atawategemea pakubwa magavana wanaomuunga mkono kama Stephen Sang (Nandi), Seneta Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet), Seneta Susan Kihika (Nakuru), wabunge Nelson Koech (Belgut) miongoni mwa wanasiasa wengine. Wanasiasa hao watatarajiwa kudhibiti urejeo wa wimbi la Kanu, linaloongozwa na Bw Moi.

Eneo la Nyanza na Kisii, anawategemea Naibu Gavana wa Kisii Joash Maangi, wabunge Silvanus Osoro (Mugirango Kusini), Shadrack Mose (Kitutu Masaba), Vincent Kemosi (Mugirango Magharibi) kati ya wanasiasa wengine. Duru zinaeleza Dkt Ruto pia amepata uungwaji mkono wa aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Kutekeleza Katiba (CIC) Bw Charles Nyachae.

Mlima Kenya, Dkt Ruto anawategemea washirika wa karibu wa kundi la ‘Tangatanga’ kama wabunge Moses Kuria (Gatundu Kusini), Alice Wahome (Kandara), Faith Gitau (Nyandarua), Rigathi Gachagua (Mathira) kati ya wengine.

Eneo la Kaskazini Mashariki, atawategemea wabunge Aden Duale (Garissa Mjini) na Gavana Ali Roba (Mandera).

Wadadisi wanasema ikizingatiwa ratiba ya kura ya maamuzi tayari imetoka, makundi hayo mawili yanaachilia taswira ya jinsi kampeni ya 2022 itakavyokuwa.

“Bila shaka, makundi hayo mawili ndiyo yatakuwa yakitazamwa kuhusu vile yataendesha kampeni za 2022,” asema Prof Macharia Munene, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

You can share this post!

TAHARIRI: BBI: Viongozi wasitugawanye

Bayern wapepeta Dortmund na kutua kwenye kilele cha jedwali...