• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Kila Mkenya ana umuhimu mkubwa kuamua hatima ya BBI – Ruto

Kila Mkenya ana umuhimu mkubwa kuamua hatima ya BBI – Ruto

Na SAMMY WAWERU

NAIBU Rais William Ruto ameweka wazi kauli yake kuhusu ripoti ya tume ya maridhiano, BBI.

Dkt Ruto amesema mchakato wa mazungumzo ya ripoti ya tume hiyo “unapaswa kujumuisha kila mmoja”.

Amesema hayo wakati akitoa hotuba yake Jumanne, katika maadhimisho ya Mashujaa Dei 2020 katika uwanja wa Gusii, Kaunti ya Kisii.

“Rafiki yangu Raila Odinga ametueleza kuhusu reggae; ni sawa. Ila ninadhani tutakuwa na mazungumzo ya BBI yatakayojumuisha kila mmoja,” Dkt Ruto amesema.

Ametoa matamshi hayo baada ya kiongozi wa ODM, Raila Odinga wakati akihutubu katika hafla hiyo, kusema mchakato wa BBI haukuwa umesimamishwa, ila ulikuwa katika kipindi cha mapumziko tu baada ya mkurupuko wa virusi vya corona nchini.

Akionekana kulenga wakosoaji wa BBI, Bw Raila amesema mapendekezo ya tume hiyo yatasaidia kukumbuka Mashujaa waanzilishi wa taifa hili.

“Reggae ilikuwa mapumziko mafupi, wachezaji wamenyoosha viungo, sasa turudi uwanjani kwa sababu hakuna anayeweza kusimamisha reggae,” akasema waziri huyo mkuu wa zamani, akieleza kwamba Rais Uhuru Kenyatta ndiye atatoa mwelekeo kuhusu ripoti hiyo.

Aidha, Rais Kenyatta na Bw Raila wanatarajiwa kupokea wakati wowote ripoti ya BBI.

Jopokazi la kuandaa ripoti ya BBI lilibuniwa baada ya salamu za maridhiano kati ya viongozi hao wawili, maarufu kama Handisheki, Machi 2018, kwa kile waliahidi ni mchakato wa kufufua utaifa na kuua uhasama ambao ni hatari.

Aidha, salamu hizo za heri njema zilisababisha kubuniwa kwa makundi mawili ‘Kieleweke’ (linaloegemea upande wa Rais Kenyatta na Odinga), na ‘Tangatanga’ linaloegemea upande wa Naibu Rais Ruto.

Wandani wa Dkt Ruto wanahoji Handisheki na BBI inalenga kuzima ndoto zake kuingilia Ikulu 2020.

Kundi la Tangatanga limekuwa likitilia shaka uhalisia wa BBI.

Naibu Rais ameshikilia hataunga mkono mapendekezo ya kubuni nafasi zaidi za uongozi, na badala yake ataunga mkono BBI ikiwa italenga kuimarisha maisha ya Wakenya.

You can share this post!

MASHUJAA DEI: Viongozi wahutubu kwa ukomavu

Arsene Wenger ajibu maswali kuhusu Arsenal, VAR, Ozil,...