Siasa

‘Malaika’ Charargei, aharamisha vyama vya Sonko, Waititu na Gachagua

Na BENSON MATHEKA December 14th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

IWAPO tafsiri ya sheria ya baadhi ya viongozi itaruhusiwa, basi kuna wanasiasa haramu Kenya; bila hata kutambua haki ya kila raia ya kujiunga na chama cha kisiasa wanachochagua.

Haya yamejitokeza kutokana na kauli za Seneta wa Nandi, Samson Cherargei, ambaye amekemea vikali Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) kwa kuidhinisha chama kipya cha aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Mike Sonko, cha National Economic Development Party (NEDP).

Mbali na Sonko, Bw Cherargei alitaja viongozi anaohisi kuwa hawafai kuunda na kuongoza vyama vya kisiasa humu nchini.

Katika taarifa aliyochapisha wiki hii katika mitandao yake ya kijamii, Bw Cherargei alisema kuwa Sonko, aliyekuwa Gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu, na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, wote waliowahi kuondolewa mamlakani kupitia mchakato wa kuwatimua, sasa wana vyama vya siasa, jambo ambalo alisema ni kinyume cha sheria.

Ni muhimu kutambua kwamba aliotaja wote wanahusishwa na upinzani. Kwa mujibu wa Cherargei, viongozi waliochunguzwa na kuondolewa mamlakani hawana haki ya kisheria kuunda au kuongoza vyama vya siasa licha ya Katiba kuruhusu uhuru wa kisiasa.

Ni muhimu kukumbuka kuwa Bw Cherargei ni wakili anayejua wazi kwamba Katiba inaruhusu kila raia wa Kenya kujiunga na chama cha kisiasa anachopenda.

Alitaja hatua ya ORPP kuwa ya kushangaza, isiyo halali, kinyume cha Katiba na ishara ya “ufisadi wa kiwango cha juu.”

Kulingana na Seneta huyo, Msajili wa Vyama vya Kisiasa amevunja sura ya katiba kuhusu uongozi na maadili, na anapaswa kuwajibishwa kisheria.

Akizungumza baada ya kuzindua chama hicho Jumanne, Desemba 9, 2025, Sonko alisema NEDP inalenga kutoa uongozi mbadala kwa nchi, akidai kuwa Kenya imekwama kwa vyama ambavyo havijawahi kuwapa Wakenya suluhu ya maana.