Siasa

Mashtaka dhidi ya Malala yaondolewa

August 18th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

SHABAAN MAKOKHA na CHARLES WASONGA

SENETA wa Kakamega Cleophas Malala aliachiliwa huru Jumanne asubuhi baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Nordin Haji kuondoa mashtaka dhidi yake.

Bw Malala ambaye alikamatwa nyumbani kwake Kitengela Jumatatu asubuhi na kusafishwa kwa zaidi ya saa nane hadi kituo cha polisi cha Mumias ambako alikesha hadi Jumanne asubuhi.

Wakili wake Charles Malala alithibitisha kuwa mteja wake aliachiliwa huru baada ya Bw Haji kuingilia kati.

Seneta Malala alikamatwa kwa madai kuwa alihutubia mkutano wa hadhara mjini Mumias Jumapili alipoongoza shughuli ya kusambaza sanitaiza kwa wanawake wajane.

Maafisa wa Idara ya upelelezi (DCI) walisema kuwa kitendo hicho ni kinyume cha masharti ya Wizara ya Afya ya kuzuia kusambaa kwa virusi vya corona.

Wananchi walifanya maandamano mjini Mumias Jumanne asubuhi wakipinga kukamatwa kwa Bw Malala.

Huku wakiimba “No Malala No Peace” (Hakutakuwa na amani bila Malala) watu hao wengi wao wakiwa vijana waliteketeza magurudumu katika mji wa Mumia huku wakikabiliana na maafisa wa polisi wa kupambana na fujo.

Baada ya kuachiliwa huru, Seneta Malala alihutubia umati mwengine katika uwanja wa Bomani mjini Mumias lakini maafisa wa polisi wakauvuruga kwa kutumia vitoa machozi.

Bw Malala alikariri kuwa hatabadili msimamo wake wa kupinga mfumo wa ugavi wa fedha baina ya kaunti ambao utapelelekea kaunti zingine kupoteza na zingine kufaidi.

Maseneta wa mrengo wa Team Kenya, ambao pia wanapinga mfumo huo, Jumatano walishikilia kuwa Bw Malala na maseneta Christopher Lang’at (Bomet) na Stephen Lelengwe (Samburu) walikamatwa ili kutokana na msimamo wao kuhusu suala hilo.