Siasa

Matiang'i na Kibicho mwiba kwa Naibu Rais

August 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BENSON MATHEKA

HATUA ya Rais Uhuru Kenyatta ya kumuongezea mamlaka Waziri wa Usalama wa Ndani, Fred Matiang’i na katibu wa wizara hiyo Dkt Karanja Kibicho kwa kuweka idara zaidi muhimu chini ya wizara wanayosimamia itawakosesha usingizi wandani wa Naibu Rais William Ruto.

Washirika wa kisiasa wa Dkt Ruto chini ya vuguvugu la ‘Tangatanga’, wamekuwa wakilalamika kuwa, lengo la kumkweza Dkt Matiang’i ni kumhujumu Naibu Rais na kumwekea vikwazo katika azma yake ya kugombea urais ifikapo mwaka 2022.

Mnamo Ijumaa, Rais Kenyatta aliweka idara ya uhamiaji chini ya usimamizi wa katibu wa wizara ya Usalama wa Ndani Dkt Karanja Kibicho ambaye wanachama wa ‘Tangatanga’ wamekuwa wakimlaumu kwa kumhujumu Dkt Ruto.

Rais alisema alichukua hatua hiyo kuimarisha utendakazi, uwazi na uwajibikaji.

“Serikali yangu imejitolea kuimarisha utendakazi, uwazi, uwajibikaji kupitia mfumo wa utawala unaohakikisha Wakenya katika sehemu zote za nchi wanapata huduma,” alisema Uhuru.

Idara ya Uhamiaji haikuwa na katibu tangu Gordon Kihalangwa alipohamishiwa Wizara ya Ulinzi mwezi Julai.

Wizara hiyo sasa itakuwa ikijulikana kama Usalama, Uhamiaji wa Ndani na Huduma za Raia.

“Kuna haja ya kulainisha majukumu ya wizara kadhaa, idara na mashirika ya serikali ili kuharakisha utekelezaji unaoendelea wa ruwaza ya kubadilisha Kenya kuwa bora zaidi chini ya Ajenda Nne Kuu,” alisema Rais kwenye agizo lake.

Julai 2019 wandani wa Dkt Ruto walimlaumu Dkt Kibicho kwa kushirikiana na baadhi ya mawaziri kutoka Mlima Kenya kupanga njama za kumuua Naibu Rais.

Dkt Kibicho, mawaziri Peter Munya, Sicily Kariuki na Joe Mucheru walipuuza madai hayo.

Uhusiano ‘usioridhisha’ kati ya Dkt Matiang’i na Dkt Ruto ulianza kujitokeza mapema mwaka 2019 Rais Kenyatta alipomteua waziri huyo kusimamia kamati ya baraza la mawaziri ya maendeleo na mawasiliano.

Ukaguzi wa miradi ya maendeleo

Wandani wa Naibu Rais walihisi kwamba hatua hiyo ililenga kuzima ziara zake za kukagua miradi ya maendeleo maeneo mbalimbali ambako siasa zilitawala.

Katika hatua ya kuhakikisha Dkt Matiang’i na Dkt Kibicho watakuwa na mamlaka zaidi kuhusu miradi ya serikali, Rais Kenyatta alihamishia kitengo cha kufuatulia utendakazi katika ofisi yake kutoka Ikulu hadi wizara hiyo mpya.

Kitengo hicho maarufu kama Presidential Delivery Unit kilikuwa kikisimamiwa na Mkuu wa Wafanyakazi wa Ikulu Nzioka Waita.

Dkt Matiang’i pia atakuwa akisimamia idara ya uwiano wa kitaifa ambayo ilikuwa chini ya ofisi ya Rais.

Hii inampatia mamlaka ya kukabiliana na wanasiasa wanaozua chuki za kikabila. Kwenye agizo la Ijumaa, Rais Kenyatta alihamisha idara ya unyunyuziaji maji mashamba kutoka wizara ya Kilimo inayosimamiwa na Bw Mwangi Kiunjuri, mmoja wa wandani wa Dkt Ruto eneo la Mlima Kenya.

Bw Kiunjuri ni waziri wa pekee kutoka eneo hilo ambaye hakutajwa katika madai ya njama za kutaka kumuua Dkt Ruto.

Idara ya Unyunyuziaji maji mashamba itakuwa chini ya Wizara ya Maji na Usafi inayosimamiwa na waziri Simon Chelugui.

Hatua hii ilijiri wakati ambao miradi kadhaa ya ujenzi wa mabwawa imekumbwa na madai ya ufisadi wa mabilioni ya pesa.