Mikutano ya BBI kuisha Machi – Raila
DICKENS WASONGA na GAITANO PESSA
KIONGOZI wa ODM Raila Odinga alitangaza Jumamosi kuwa mikutano ya uhamasisho kuhusu yaliyomo kwenye ripoti ya mpango wa maridhiano (BBI) itafikia kikomo Machi kuelekea hatua ya mwisho ya kura ya maamuzi.
Bw Odinga alisema baada ya hapo, afisi kuu ya BBI itaanza kampeni ya kukusanya sahihi milioni moja kote nchini.
Akiongea wakati wa mazishi ya aliyekuwa naibu kamishna wa polisi katika kijiji cha Magadini, eneo bunge la Ugenya, Raila alisema baada ya hapo mswada kielelezo utawasilishwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) uidhinishwe kutoa nafasi kwa matayarisho ya kura ya maamuzi.
Ufichuzi huo unajiri baada ya wanasiasa kutumia mikutano ya uhamasisho kuhusu BBI iliyoanza Januari mjini Kisii kuipigia debe mageuzi ya Katiba kupitia kura ya maamuzi.
Seneta wa Siaya James Orengo ambaye ni mwandani wa Odinga ameitaka kamati ya BBI kuandaa Mswada wa marekebisho ya vifungu vya Katiba kwa maandalizi ya kura ya maamuzi kabla ya Julai.
Awali, katika eneobunge la Matayos, Busia ambako alihudhuria mazishi ya aliyekuwa mwanachama wa bodi ya nafaka na mazao (NCPB) Mzee John Melti Okinda, Odinga alisema changamoto zinazokabili taifa hili zinaweza tu kusuluhishwa kwa kutekeleza ajenda tisa za BBI.
Changamoto hizo ni kama vile ufisadi, ukabila na ukosefu wa ajira.
Bw Odinga alisema jopokazi la BBI linaweza kuwafikia wananchi moja kwa moja badala ya kufanya vikao sehemu mbalimbali nchini.
“Tunataka shughuli za mashauriano na uhamasisho zikamilike kufikia Machi kabla ya kuanza kutekeleza yaliyomo katika ripoti ya BBI kupitia bunge au kura ya maamuzi,” akasema.
Bw Odinga alisema hayo huku viongozi kutoka eneo la Magharibi mwa Kenya wakiunga mkono mpango wa BBI.
Vilevile, walipendekeza kuwa nafasi zaidi za uongozi zibuniwe katika Katiba.
Viongozi hao; Moses Wetang’ula (Bungoma), James Orengo (Siaya), Amos Wako (Busia), Gavana wa Busia Sospeter Ojaamong, na wabunge Geoffrey Odanga (Matayos), John Bunyasi (Nambale), Florence Mutua (Mbunge Mwakilishi wa Wanawake Busia) na aliyekuwa Mbunge wa Westlands Fred Gumo walimhakikishia Bw Odinga kuwa eneo hilo linaunga BBI.